Study in South Africa: (www.southafricauniversities.blogspot.com) or Uganda: (www.ugandauniversities.blogspot.com)

Pages

Wednesday, October 16, 2013

Vijana wanavyopaswa kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere

NA CHRISTOPHER NGUBIAGAI.

OKTOBA 14 kila mwaka Watanzania huungana kuadhimisha siku ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ili kutoa fursa kwa watu mbalimbali hasa vijana kujifunza juu ya ujasiri, uadilifu na uzalendo kwa faida ya wote.

Mwalimu Nyerere aliaga dunia Oktoba 14, 1999 baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kuanzia wakati huo Watanzania wamekuwa wakitumia siku hiyo kuadhimisha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambapo mwaka huu, Taifa linatimiza miaka 14 bila ya kiongozi huyo mashuhuri na mwenye sifa ya kipekee kwa kutetea wanyonge na mpigania haki asiyetetereka wala kuyumbishwa.

Ingawa pengo lililoachwa na Mwalimu Nyerere haliwezi kuzibika, vijana wanapaswa kufuata nyayo za kiongozi huo Muasisi wa Taifa ili kujenga moyo wa ujasiri, uadilifu na uzalendo na kuwa mstari wa mbele kulinda nchi na mipaka yake. Katika milenia hii ya sayansi na teknolojia, vijana wa kike na kiume ni rasilimali kubwa zaidi kwa sasa na siku za baadaye.

Wanatoa msukumo wa kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi na kisiasa katika eneo lenye mabadiliko ya haraka duniani. Pamoja na mambo mengine, maendeleo ya Taifa lolote yanategemea zaidi makuzi na maandalizi ya vijana kwa ajili ya maisha ya kujitegemea na kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii, kiutamaduni, na kiuchumi.

Wataalamu wa masuala ya maendeleo wanasema ili Taifa liweze kuendelea ni muhimu kuwaandaa vijana kuwa viongozi, watoa maamuzi, wajasiriamali, wazazi na walezi wazuri. Matokeo ya sensa ya mwaka 2012 yanathibitisha ongezeko la vijana wa Tanzania na ambapo kwa takwimu zinaonesha vijana walio kati ya miaka 15 na 35 ni zaidi ya milioni 15, hii ni sawa na zaidi ya asilimia 34 ya Watanzania wote.

Ni wazi kuwa ongezeko la vijana linaweza kusababisha mageuzi makubwa katika uwanja wa siasa na chaguzi zijazo ambapo wapiga kura wengi watakuwa wamezaliwa kipindi ambacho Mwalimu Nyerere alikuwa keshaondoka madarakani. Vijana wanapaswa kufundisha na kujifunza uzalendo ikiwa na maana hali ya mtu kuipenda na kuithamini nchi yake na kuweka maslahi ya taifa lake mbele.

Uzalendo ni neno dogo fupi lenye kubeba maana nzito. Ukosefu wa mafunzo juu ya uzalendo unasababisha baadhi ya watu kutokujiamini, kukataa mila na desturi za makabila yao, kukana kabila pia kutamani kuwa mtu wa taifa lingine.

Vijana wanapaswa kuiga mfano wa Mwalimu Nyerere ambaye alipuuza maendeleo ya magharibi na kuzungumzia maendeleo yetu wenyewe ingawa nchi ilikuwa imetapakaa nyumba za tembe ama msonge, watu wakitembea bila mavazi wala viatu na hapakuwa na Watanzania wanaomiliki magari wala chombo cha moto.

Nyerere ambaye alikuwa msomi wa Chuo Kikuu wakati huo alikataa ukoloni mambo leo, na akatangazia taifa kujenga umoja na mshikamano kumng’oa mkoloni ili kuwafanya Waafrika kuwa huru na kujiamulia mambo yao wenyewe bila kuingiliwa wala kugandamizwa na mataifa mengine.

Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni muafaka kutafakari na kuweka mikakati ya kuendeleza mazuri yaliyoachwa na kiongozi huyo, aliyewasha taa na ili kila mtu apate kuona kisha akaweka misingi imara ya Taifa. Mwalimu Nyerere alitumia lugha ya Kiswahili kuunganisha Watanzania ili kuondoa kikwazo cha mawasiliano baina ya makabila zaidi ya 130 kwa lengo la kuongeza umoja na mshikamano na kupunguza hali ya kutokuelewana.

Kila kabila lina maadili yake, lakini maadili ya taifa yaliwekwa rasmi na waasisi wa taifa hili wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na kutolewa kwa wananchi kwa mara ya kwanza kama ahadi za TANU na kurithiwa na Watanzania bila kujali itikadi za kisiasa, kabila wala dini.

Ahadi hiyo inasema: binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja, nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote, nitajitolea nafsi yangu kuondoa ujinga, umasikini na maradhi, rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa. Cheo ni dhamana sitakitumikia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.

Pia ahadi hiyo inasema nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote, nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yangu na nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko. Ingawa hivi sasa kuna mfumo wa vyama vingi hakuna ukakika kama kuna chama chochote chenye mapenzi mema na Taifa hili kinachoweza kwenda kinyume na ahadi hiyo.

Hivyo vijana wanapaswa kushikamana na kuendeleza misingi ya maadili mazuri yaliyowekwa na Mwalimu Nyerere bila kujali tofauti za idikadi zao kisiasa wala kidini. Msomi mmoja wa Kigiriki aliwahi kusema katika mwaka 560 BC kuwa mfanyabiashara anafanya vizuri kwa kukubali kupata hasara kuliko kupata faida haramu kwa sababu hasara inaweza kuuma au kwa muda mfupi lakini faida haramu inauma milele.

Kama anavyoainisha Kaduma, katika kitabu chake, maadili ya Taifa na Hatima ya Tanzania, kwa ujumla wake ahadi hizi zinalenga kumuandaa Mtanzania ili awe mtu mwenye upendo, mwaminifu na mtiifu, awe mtumishi bora wa umma, ajielimishe kwa bidii na kisha atumie elimu hiyo ili alete maendeleo kwa taifa zima.

Zinamtaka Mtanzania awe mkweli na muwazi, akatae kutoa wala kupokea rushwa, apambane kwa bidii zake zote na maadui watatu wa taifa hili yaani, Ujinga, Umasikini na Maradhi. Ingawa maadili kama haya ni muhimu kwa taifa lolote lile ni dhahiri ni muhimu zaidi kwa taifa changa kama letu.

Hata hivyo, nchi yetu imepata matatizo kwa sababu baadhi ya Watanzania hatujawa waaminifu katika kutekeleza ahadi hizo muhimu, hivyo hata baadhi ya viongozi wetu wanashindwa kukemea uovu. Ni vijana wangapi leo hapa Tanzania wanaotamani kuwa na mikono misafi watakapoanza kazi kama watumishi wa umma au viongozi kama sehemu ya kumuenzi Mwalimu Nyerere?

Ni wakati muafaka wa kujiuliza na kuweka mikakati sahihi ya kuendeleza Taifa badala ya kujiweka katika ulimwengu wa utandawazi ambao mara zote hutoa matumaini makubwa na kuwafanya vijana kujenga matumaini ya kufikirika kupitia mitandao ya kompyuta. Ingawa utandawazi unawapa matarajio vijana, utandawazi huo hautoi nyenzo sahihi za kuwapatia uwezo na fursa vijana ya kuitimiza ndoto zake.

Vijana wa leo tunapaswa na tunalazimika kufungua macho na bongo zetu tujifunze kwa bidii na kwa haraka sana na hatimaye tuungane kuhuisha misingi imara ya uongozi iliyojengwa na Mwalimu Nyerere. Hilo ni jukumu la msingi la vijana katika kumuenzi Mwalimu Nyerere na kama kizazi chetu kinataka kuepuka laana ya Mwalimu Nyerere.

Mwalimu Nyerere katika kitabu chake, “Uhuru na Ujamaa, 1968”, alisema katika ukurasa wa 33 kama ifuatavyo: “Kila kizazi kina changamoto zake na kila kizazi kinapaswa kutumia fursa walizonazo kujiletea maendeleo na kufanya maisha bora.” Fursa ya kuleta maendeleo kwa maisha ya Mtanzania ni mabadiliko kutoka katika mfumo na sera kwa ajili ya wakati na mazingira yaliyopo.

Baadhi ya changamoto zinazowakabili vijana ni ukosefu wa ajira, rasilimali na nafasi ya kufanya maamuzi. Hata hivyo, baadhi ya vijana hawatambui nafasi wala wajibu wao katika taifa hivyo siku ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inapaswa kutumika kuelimisha vijana hao na jamii nzima umuhimu wa ujenzi wa Taifa.

Tatizo hili la kutokujitambua linaambatana na tatizo kuu la kutojiamini. Kutokujiamini ndio adui mkubwa wa maendeleo ya kijana na Taifa kwa ujumla na limezuia mabadiliko chanya ambayo yangeweza kutokea ili kulijenga taifa letu.

Katika kuenzi fikra za Mwalimu, wakati umefika vijana wote tusimame imara, sisi ndio nguvu kazi ya taifa hili, tujipange vema na hasa kwa wale vijana ambao wana nafasi za uongozi katika nyanja mbalimbali tuweze kuijenga nchi yetu na kutoa mchango mwetu kama vijana wazalendo wa taifa hili.

Mwlimu Nyerere katika kitabu cha Uhuru na Ujamaa, (1968), uk 167 anakemea suala zima la ubinafsi na hasa kwa wakati tuliyo nao. Hii ni changamoto kubwa sana na ina uhusiano wa karibu na ile ya kwanza. Watu wengi tumefikia kudhani kwamba ukipata wewe na familia yako imetosha. Watanzania tumekuwa na roho za kutojaliana, unajifikiria mwenyewe tu.

Yafaa nini kupata mali, kuwa na vitu vya thamani sana na kula vyakula vya gharama, lakini mtanzania mwenzako hawezi hata kujikimu kwa siku. Hayo nayo utayaita ni mafanikio? Hapana, huo ni ubatili na kujilisha upepo! Jaribu kuchukua mfano wa Mtu kama Nelson Mandela, angeweza kupata maisha mazuri sana kama angeamua kutafuta ugali wa familia yake tu.

Kumbuka aliwahi kuambiwa na makaburu aachiwe huru lakini asijihusishe na siasa, akakataa. Akakaa jela miaka 27. Viongozi wa Tanzania kuanzia kizazi cha Mkwawa na Nyerere walilipia sadaka, hawakuogopa kupoteza au familia zao kuteseka, hawakuwa wabinafsi. Bila Mandela kujikana, labda leo Afrika Kusini ingekuwa bado chini ya makaburu.

Vijana lazima tuache ubinafsi, tuiangalie Tanzania, watu wote wa Tanzania, tusijikwamue wenyewe kimaisha tukawasahau wenzetu wasio hata na fursa ya kupata elimu.

Tuna mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa Mwalimu Nyerere; lakini kikubwa ni kuthubutu na kupigania mabadiliko chanya ya kweli bila kusita wala kujali maslahi binafsi bali ya watanzania kwa ujumla wa kizazi cha sasa na kizazi kijacho. Mwandishi wa makala haya ni msomaji wa HabariLeo.

Credit to: http://www.habarileo.co.tz/index.php/makala/17527-vijana-wanavyopaswa-kufuata-nyayo-za-mwalimu-nyerere

No comments:

Post a Comment

© 2012 Designed by My Blogger Tricks