Study in South Africa: (www.southafricauniversities.blogspot.com) or Uganda: (www.ugandauniversities.blogspot.com)

Pages

Thursday, October 10, 2013

MCHAKATO WA KATIBA MPYA: Tujikumbushe pia Azimio la Arusha

“MIMI bado natembea nalo (Azimio la Arusha). Nalisoma tena na tena sioni kasoro na sioni cha kubadili. Labda ningeboresha Kiswahili nilichokitumia, lakini Azimio lenyewe bado ni thabiti. Nisingebadili hata neno moja,” anasema Mwalimu Julius Nyerere alipoongea na waandishi wa habari mwaka 1999.

Mwalimu anasema, inaweza kuwa vigumu kuzungumzia ujamaa, lakini anashangaa tulivyotelekeza moja ya dhana nyingine ya Azimio la Arusha ambayo ni ‘Kujitegemea’. Naam, hilo ndilo Azimio la Arusha lililopishwa miaka 47 iliyopita. Ilikuwa Februari 5, mwaka 1967 pale Rais wa TANU, Mwalimu Julius Nyerere alipotangaza hadharani kupitishwa kwa Azimio la Arusha kwa lengo la kuleta mageuzi ya haraka na kutoa mwelekeo mpya wa nchi.

Azimio hilo lilipitishwa baada ya kukubaliwa kwenye Mkutano Maalumu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Tanganyika African National Union (TANU). Kitabu cha Uamuzi wa Busara cha TANU kinachoelezea mambo muhimu ya historia ya nchi yetu, kinaainisha pia mambo muhimu ambayo kama yasingefanywa historia ya nchi yetu isingekuwa ilivyo leo.

Kitabu hicho kinaeleza kuwa haikuwa rahisi kulipitisha Azimio hilo kwa kuwa viongozi wengi wa TANU na Serikali walikuwa wameanza kuona uzuri wa kuwanyonya wananchi. Yaani baada ya kupatikana kwa uhuru kutoka kwa wakoloni, sasa watawala wapya walitaka kuvaa viatu vya wakoloni wale wale kwa maana ya kufaidi keki ya taifa peke yao bila kuangalia maslahi mapana ya wananchi.

Katika mkutano wa kujadili kupitisha au kutopitisha Azimio hilo, majadiliano makali yaliendeshwa na inaelezwa kwamba wengi wa wajumbe walikuwa hawaelewi kwa nini TANU ilikuwa imependekeza Azimio hilo. Hata hivyo, baadaye walielewa sababu za kutaka litipishwe na ndipo wajumbe wakaona umuhimu wa kuwepo kwa Azimio hilo, ili kuleta ukombozi na maendeleo kwa wananchi.

Azimio la Arusha ni nini? Azimio la Arusha ni tamko rasmi la Chama cha TANU linaloelezea jinsi nchi itakavyoendeshwa kwa kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Msingi wake mkubwa ni imani katika haki na Usawa kwa Binadamu Wote! Azimio hilo linaitwa la Arusha kwa sababu Arusha ndipo majadiliano yote hadi kufukia uamuzi wa kulitangaza rasmi yalipofanyika, na kuwa jina Arusha linatumika kama ukumbusho wa mahali lilipopitishwa.

Katika kitabu hicho inaeleza kuwa Azimio hilo ni kwa wananchi wote wa Tanzania Bara. Aidha chanzo cha kuwepo kwa Azimio hilo ni kukazia mambo yaliyopo kwenye Katiba ambayo hayakutiliwa mkazo kutokana na sababu mbalimbali. Usawa wa binadamu Baadhi ya sababu ni kama kusisitiza usawa baina ya binadamu wote.

Awali wakati wa utawala wa serikali ya kikoloni, utu wa mtu ulithaminiwa kulingana na rangi yake. Mwafrika alikuwa mtu wa mwisho kwa thamani kutokana na rangi yake nyeusi ambapo Mzungu alionekana ni mtu wa thamani kuangalia rangi yake na Mhindi naye akafuatia, hivyo utu wa mtu ulipimwa kwa kuangalia rangi, jambo ambalo sio sahihi kwani Katiba inasema binadamu wote ni sawa.

Hivyo Azimio la Arusha liliingia kuondoa udhalilishaji na unyimwaji haki kwa kuangalia rangi ya mtu, na kwamba Wazungu, Wahindi walisahau kuwa hata Waafrika ni binadamu na hivyo TANU ikapigana kuhakikisha uhuru unapatikana ili kuweka usawa na haki kwa kila mtu.

Katiba inaeleza kuwa kila binadamu anastahili heshima, TANU ilipigana na mkoloni ili kurudisha heshima na kwamba hakuna heshima yoyote ikiwa taifa lolote litatawaliwa na taifa jingine. Hivyo Azimio la Arusha likatangazwa kurejesha heshima ya kila mtu hususan Mwafrika.

Azimio hilo linatamka katika ukurasa wa tano: “Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa.” Ni wazi kuwa Azimio hilo lililenga katika kuwatoa Watanzania katika hali ya unyonge, kunyonywa na kupuuzwa na ndiyo maana azimio hilo linapinga aina yoyote ya dhuluma na uonevu.

Unyonyaji Kitabu hicho kinaeleza kuwa sehemu ya kwanza ya Imani ya TANU inaelewa wazi kuwa ni wajibu wa Serikali ambayo ndiyo watu wenyewe kuhakikisha maisha ya uchumi wa taifa pamoja na watu wake unaimarika na kuzuia aina yoyote ya unyonyaji baina ya watu.

Aidha kinaeleza kuwa Serikali inawajibu kuzuia watu kujilimbikizia utajiri kiasi cha kutopatana na siasa ya watu wote kuwa sawa, hivyo Azimio hilo linaingia ili kukumbusha hayo ambapo yalianza kuonekana kukiukwa na hivyo kutoleta usawa wala heshima kwa binadamu.

Kitabu hicho kinaendelea kueleza kuwa, Azimio la Arusha lilikuwa na maana nzuri, lilitaka uchumi wa taifa uwanufaishe watu wote, lakini hali halisi ya sasa ni kuwa kuna sehemu kubwa ya uchumi wa nchi yetu uko mikononi kwa watu wachache.

Hali hii inakuwa mbaya kadri siku zinavyosonga kwani wachache ndio wenye mali nyingi huku kundi kubwa la Watanzania likibaki masikini, jambo ambalo ni unyonyaji, na kwamba msingi wa Azimio ni kuleta usawa kwa binadamu wote.

Je hilo linawezekana, ikiwa leo hii kuna watu miongoni mwetu hawana uhakika wa kula wakati wengine wanakula na kusaza? Jambo jingine muhimu ambalo Azimio la Arusha lilimulika ni rasilimali za taifa. Katiba inasema raia wa Tanzania watamiliki utajiri wa asili wa nchi yao na kwamba umiliki huo uwe dhamana kwa vizazi vijavyo.

Lakini wakoloni walipotawala pole pole wakajinyakulia ardhi na kuifanya yao. Hata hivyo, waliwatumikisha wazalendo na walitumia pia mbinu mbalimbali kuwagawa na kuwafarakanisha watu hasa pale walipoona wananchi wanadai haki zao. Hata hivyo, baada ya uhuru baadhi ya viongozi walisahau machungu na vidonda vya ukoloni, wakaanza kujilimbikizia mali na kuwanyonya wananchi wenzao, jambo ambalo liliwakera wananchi na kuhoji; sasa kuna afadhali gani kupata uhuru?

Waliona maisha ni sawa na enzi za mkoloni na hata baada ya mkoloni, hivyo hiyo ikawa chachu ya kuhakikisha Azimio la Arusha linatangazwa ili kurudisha imani, utu, na nidhamu ya watu na masuala yote ya umiliki ardhi, uchumi na hata uzalendo. Baada ya Azimio kutangazwa mambo yakabadilika, utu ukarejea, uchumi ukaondoka mikononi mwa wachache na wananchi wakaona kweli ni siasa ya ujamaa na kujitegemea.

Azimio hilo ambalo lilisimamiwa na Mwalimu Nyerere, linaelezwa kufifishwa na mwaka 1991 baada ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukutana Zanzibar na kufanya mabadiliko ya azimio hilo. Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi wakati akiwa madarakani alisema Azimio la Arusha halikusudiwi kufa ila linafanyiwa maboresho ili liendane na hali ya wakati uliopo.

Alisema, “Halikugeuka wala hatutazamii kuligeuza. Kwa hali yoyote sisi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi hatutaweza kuigeuza siasa hii. Kule Zanzibar tulizungumza mengi, miongoni mwao ni kutoa tafsiri ya baadhi ya vipengele vya Azimio ili vifanane na wakati tulionao.” Akifafanua zaidi, Mwinyi anasema tangu azimio hilo lilipoanzishwa mwaka 1967 hadi mwaka 1991 ilikuwa imepita zaidi ya miaka 20, hivyo kulikuwa na mabadiliko mengi duniani. “Hali yetu ya sasa hasa ya kiuchumi, siyo ile ya mwaka 1967.

Ndiyo maana mishahara ya wafanyakazi ingawa imeongezeka sana, lakini bado haikidhi mahitaji yao, haiwatoshi hata wale wanaopokea mishahara mikubwa miongoni mwetu,” anasema na kuongeza: “Isitoshe, wakati wa Azimio idadi ya Watanzania ilikuwa ndogo, sasa hivi idadi yetu imeongezeka zaidi ya mara mbili.

Kwa sababu ya wingi wetu, mahitaji yameongezeka sana, wakati mapato yetu yamekuwa yakipungua wakati wote.” Mwinyi anaongeza kuwa kila zama na mwongozo wake: “Msahafu wa Waislamu unasema “Likulli ajalin kitab’, yaani kila zama ina kitabu chake,” anasema na kuongeza: “Sisi wana CCM tunakubali kuwa kila zama zinahitaji kuwa na mwongozo wake. Azimio la Arusha ni mwongozo wetu wa msingi.

Ni dira inayoongoza mwelekeo wa jamii yetu. Lakini tafsiri zake inabidi zirekebishwe kila inapohitajika ili zisipitwe na wakati. Hata hivyo Mwalimu Nyerere hakuridhika na msimamo wa CCM, na alisema hajaona kasoro ya Azimio hilo pale alipoongea na waandishi wa habari mwaka 1999.

Lakini, kuna watu ambao wanadhani kwamba yapo ya msingi tunaweza kuyahifadhi yaliyo ndani ya Azimio la Arusha hata kama si kulirejesha kabisa kama lilivyokuwa. Hilo linathibitishwa pia na aliyekuwa Waziri Mkuu, Jaji mstaafu Joseph Warioba, ambaye katika moja ya maneno yake alisema anatamani Azimio la Arusha lirudi kwa kile alichosema hivi sasa kuna mmomonyoko wa maadili kwa viongozi wengi.

Credit to: IKUNDA ERICK (http://www.habarileo.co.tz/index.php/makala/15965-tunapojadili-katiba-tujikumbushe-pia-azimio-la-arusha-lililenga-nini)

No comments:

Post a Comment

© 2012 Designed by My Blogger Tricks