Study in South Africa: (www.southafricauniversities.blogspot.com) or Uganda: (www.ugandauniversities.blogspot.com)

Pages

Friday, October 11, 2013

Azimio la Arusha la nini, tuna Utandawazi

Na Ayub Rioba.

WAKATI tukielekea Kilimanjaro Hoteli kuhudhuria mkutano wake na waandishi wa habari, hatukutarajia kwamba sisi wenyewe waandishi tungekosa pahala pa kusimama.

Mwaka 1995 Mwalimu Julius Nyerere alikuwa amekwishatoka madarakani na alikuwa akifanikiwa sana kuona makosa ya walio madarakani kwa wakati huo. Mikutano yake ilikuwa na mvuto kiasi kwamba wahudhuriaji walikuwa si waandishi peke yake.

Wakati akiendelea na hotuba alifika pahala akalikumbuka Azimio la Arusha na misingi yake. Akatoa siri pale ukumbini kwamba yeye siku zote alikuwa akitembea na vitabu viwili - Biblia na Azimio la Arusha. Akawachekesha waandishi na wengine waliokuwa wakimsikiliza akisema yeye alikuwa akikasoma kale kakitabu (Azimio la Arusha) na kurudia na kurudia, lakini hakupata kubaini tatizo la misingi yake.

Lakini Mwalimu alikuwa hodari sana wa kuchagua maneno. Akasema siku hizi kulizungumzia Azimio la Arusha ni lazima uwe na akili ya mwendawazimu.

Profesa wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Issa Shivji kwa mara nyingine tena ameandaa Tamasha la Kitaaluma la Mwalimu Julius Nyerere na kwa mwaka huu mada kuu ni kutafakari juu ya Azimio la Arusha na misingi yake.

Kwa muda mrefu sasa kuna watu wamejaribu kulihusisha Azimio la Arusha na umaskini. Wakakumbuka enzi zile za Ujamaa jinsi watu walivyokuwa wakijipanga kununua mahitaji muhimu kuanzia sabuni, chumvi, nguo, mafuta n.k.

Wanalinganisha na sasa wanaona kweli Ujamaa ulikuwa mfumo wa hovyo na Azimio la Arusha lilizuia watu wasiwe matajiri. Wanatizama viambazani kila pahala wanaona nguo za mitumba zimejaa, zikiwamo sidiria, soksi na chupi zilizoagizwa kutoka nje.

Wanaangaza madukani na kuona maduka yote yalivyofurika kila kitu kinachohitajika – tena basi vitu karibu vyote kutoka nje. Leo hii kwa jinsi tulivyoendelea hatuhitaji tena masoko kama ya Ubungo, Mwenge, Manzese, Tandika, ambayo mvua ikinyesha mnatafutana. Leo hii kuna supamaketi. Kila kitu mumo kwa humo. Na tena kila kitu toka nje.

Leo hii kuna watu ukiwaeleza kwamba kuna mambo mengi ya maana, ya msingi na ya kifikra yalifanyika nchini kutokana na Azimio la Arusha, wanakubishia na ikiwezekana wanakutukana.

Wanaamini kwamba hakuwezi kuwapo maendeleo ya aina yoyote kwa binadamu bila kutumia mawazo na mikakati waliyofundishwa na wakoloni wao.

Kwao wao, mfumo wa ubepari ni fomula takatifu iliyotengenezwa ikakamilika na kwamba ikiwekwa katika mtungi wowote inatoa matokeo yale yale yaliyotokea kwingineko kama ilivyo kwa sheria za sayansi.

Wanashindwa kusoma, kutafakari na kubaini jinsi mifano michache tu ya Japan, Malaysia, Korea Kusini, Botswana na kwingineko inavyotufundisha somo tofauti kuhusu ujenzi wa ubepari.

Ni kweli, na wala hili halipingiki, kwamba kwa asili binadamu huzaliwa akiwa na tabia fulani za kibepari. Lakini ni kweli kwa kiasi hichi hicho kwamba binadamu pia huzaliwa akiwa na asili ya ujamaa.

Bahati mbaya katika dunia tunayoishi leo ni ujuha uliopindukia kwetu sisi – tuliokuwa tumetawaliwa kwa muda mrefu kwa sababu ya rasilmali na nguvukazi yetu – kudhani kwamba ubepari wa dunia ndio suluhisho kwa matatizo yetu ya msingi ya umaskini, ufukara na ulofa.

Naikabili hatari ya kuonekana sijui; lakini ukweli unaoshawishi ni ule unaotuonyesha kwamba wabepari ni wale wenye mitaji iliyo juu ya ardhi.

Kwa mfano, wana akili za kutosha walizoziandaa kwa elimu bora kwa miaka mingi. Wana teknolojia iliyotokana na akili zile zile walizowekeza kuzitengeneza. Wana mitaji ya mali iliyo katika mfumo wa kibenki na mali iliyo juu ya ardhi.

Wanacho chakula cha kutosha kuhakikisha watu wao hawawi na utapiamlo katika dunia ambayo rasilmali watu ni mali kuliko dhahabu. Kisha kila kukicha wanafikiri na kubuni. Wanabuni, wanatengeneza, wanauza, wanapata faida. Na kwa kutaka faida, kila wanayekutana naye njiani katika mchakato wa kusaka faida ni lazima wamlalie.

Ndiyo maana hawamiliki migodi yetu wala mafuta yetu wanavifaidi mara nyingi kuliko sie vibarua.

Huwa ninacheka tu nikikutana na watu wakanieleza jinsi mambo yalivyobadilika tokea “tulivyoanza kufuata mfumo wa kibepari”. Ninacheka kwa sababu najua sisi kama Watanzania tutaendelea kubaki Wajamaa kwa muda mrefu sana.

Tutaendelea kukaa vikao vya harusi kuchangishana pesa kuoza watoto wetu. Tutaendelea kuombana pesa ya kula. Tutaendelea kukopana wenyewe kwa wenyewe kumaliza matatizo madogomadogo. Tutaendelea kuchangiana kila mwezi ili kila mmoja wetu apate pesa ya kutimizia mahitaji ya kila siku. Tutaendelea kusaidiana. Hao ‘mabepari’ wetu wazawa ni wachache, hawajai kiganjani.

Wabepari hatuwezi kuwa sie. Wabepari wapo. Wanajulikana kwa tabia. Wanajulikana kwa historia. Wanajulikana hata kwa rangi. Sisi ni watumishi wa mfumo wa kibepari ambao tumelazimika kufungua milango uhamie kwetu.

Kwa hiyo kudhani kwamba Azimio la Arusha lilikuwa linawachelewesha Watanzania kuwa matajiri ni kuruhusu kejeli ya kimantiki itawale namna tunavyofikiri.

Katika kujifunza historia ya nchi hii ninashawishika kuona mambo kwa mtazamo tofauti. Mwalimu Nyerere ambaye wakati mwingine hubezwa kwamba alileta umaskini na Ujamaa wake na Azimio lake la Arusha alikuwa ni mtu ambaye alikuwa anawaandaa Watanzania kuwa wabepari wa asili. Lakini bahati mbaya Watanzania wakawa na haraka.

Tulipopata uhuru tulikuwa na kila sababu ya kusherehekea. Hatukuwa tumelelewa katika mazingira ambamo watawala wetu walikuwa na rangi sawa na sisi. Tulikuwa tumeishi kwa miaka chungu nzima tukinyanyaswa, tukinyonywa, tukidhalilishwa na kupuuzwa na watu walioamini sisi hatukuwa binadamu kamili.

Waasisi wetu wakaanza uongozi kwa falsafa iliyolenga kupindua mazoea ya wakoloni. Wakabaini yale yote waliyoyapinga wakati wakipigania uhuru wakayasadifu katika tamko. Wakaazimia kujenga jamii ya watu wanaostahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wao. Wakaweka misingi kuzuia viongozi wazalendo wasitumie madaraka kama vile walivyokuwa wakiyatumia wakoloni.

Miaka ya 1980 kulikuwa na dhiki kuu kiuchumi hasa baada ya vita ya kulinda mipaka ambayo baadaye ilimuondoa Iddi Amin Uganda. Dhiki ile kwa watu wenye akili ilikuwa muhimu kuliko kitu kingine chochote. Kama ni ubepari wetu ungelianzia pale. Ilikuwa ni katika dhiki ile Watanzania walianza kujifunza kutengeneza vitu vingi kwa akili yao wenyewe na kwa mikono yao wenyewe.

Walitengeneza mafuta ya kula na ya kujipaka. Walitengeneza sabuni. Walitengeneza chumvi. Walitengeneza nguo kwa ubunifu wao wenyewe.

 Walitengeneza gongo. Walitengeneza viatu. Walitengeneza vitu vingi kwa sababu havikuwapo madukani!

Kudhani kwamba kuwa na vitu vingi toka nje, vikiwamo mitumba ya chupi na vitu feki kwa wingi, ni uamuzi bora kuliko ule wa kuruhusu watu wetu wafikiri, wabuni na kuumba vya kwao wenyewe, ni kujidhalilisha sisi wenyewe. Ni hitimisho hatari sana kwamba hatuwezi kujitegemea.

Na ndilo hitimisho ninaloliona likisadifisha hoja za wale wanaosema Nyerere alituchelewesha kuwa mabepari.

Wanashindwa kuona kwamba aliwachelewesha kuwa watumishi na vibarua (au makuwadi) wa mabepari kwa kuwataka wao wenyewe wajiandae kuwa mabepari wa asili. Lakini unyonge wetu, ule ule uliotufanya tukaonewa, tukanyonywa, tukadharauliwa na kupuuzwa wakati wa utumwa na ukoloni, sasa unatupeleka pabaya.

Hiki tunachokiita ubepari, huu wa sisi wengine vibarua wengine makuwadi; huu ubepari wa kunyang’anyana kilichopo lakini hakuna ujenzi wa akili ya kutengeneza ziada; huu ubepari wa kuagiza kila kitu toka nje na sisi hatutengenezi chochote cha maana cha kuuza nje; huu ubepari wa kutokudunduliza bali kutapanya kile kidogo tulicho nacho; huu ubepari wa kuuza kwa wawekezaji wa nje kila chenye thamani tulichopewa na Muumba wetu; huu ubepari wa kutokufikiria kesho na vizazi vijavyo; ndo ubepari sampuli gani?

Nahitimisha kwa kuweka angalizo. Mfumo wa Utandawazi ambao ndio huo huo Ubeberu wa kibepari ambao tabia zake zilijitokeza kuanzia karne tano zilizopita unazo fursa nyingi.

Wapo watu, hata katika nchi maskini kabisa wamecheza na fursa zile wamepiga hatua kubwa sana katika maendeleo binafsi. Lakini ni hatua za mtu mmoja mmoja. Sisi kama nchi hatuwezi kutelekeza mawazo yetu wenyewe tukadhani tutafanikiwa kwa mawazo yale yale ambayo kwa kipindi cha miaka mia tano sasa yametuweka hapa tulipo.

Na endapo tutapuuza mawazo yetu wenyewe basi tutambue kuwa tumehukumiwa kuendelea kuwatumikia wengine huku tukiwasaidia wao kujua kwamba sisi ni viumbe duni.

Na pale watakapokuwa wanatunyanyasa, wanatunyonya au kutudhalilisha, basi, tukae kimya kwa sababu ndiyo stahili yetu kama watu duni.

Kipo kisa kimoja cha kijana mmoja alikuwa mtoto wa Rais mmoja wa Afrika. Tulimkuta katika ukumbi mmoja jijini London mwaka 1997 akila raha. Tukaambiwa alikuwa akimiliki krediti kadi ya dhahabu. Alikuwa na makeke ya ajabu. Alifikia pahala akaamuru kila aliyekuwa ndani ya ukumbi ule anywe chochote na yeye angelipa.

Kwa mujibu wa waliomfahamu, alikuwa akiishi kwa anasa iliyopindukia. Kwa kifupi, alikuwa akiwakilisha ubepari wa nchi zetu. Kwamba unakuta maisha yao yote walikuwa watu wa kawaida kabisa, tena watumishi tu. Lakini familia za Kiafrika zikishapata madaraka tu, ghafla Rais anakuwa bepari, mke bepari, watoto mabepari n.k. Lakini kabla hawajashika madaraka hata genge la nyanya hawakuwahi kuwa nalo. Na ubepari wao huwa ni wa aina moja tu. Hauwezi hata siku moja kukuta ubepari uliotokana na ubunifu kama wa Bill Gates au wa wale watoto walioanzisha Facebook huko Marekani.

Wakati mtoto yule wa rais wa Afrika akiendelea kuchezea mali ya walipa kodi wa nchini kwake, rafiki yangu wa kule aliniuliza: Hivi Ayub huyu ndugu yenu kama ana pesa kiasi hicho si akawasaidie nduguze huko kwenu wanaokufa kwa njaa na maradhi yanayotibika? Ameona kuna mtu anakufa njaa hapa? Hakuna atakayemheshimu hapa kwetu eti kwa sababu ya matumizi yake makubwa; watu wa hapa wanamtazama kupitia miwani ya wale watoto wenye tongotongo na wanaokufa kwa njaa kule Afrika tunaowaona katika televisheni kila siku! Azimio la Arusha?

Credit to: http://www.raiamwema.co.tz/azimio-la-arusha-la-nini-tuna-utandawazi

No comments:

Post a Comment

© 2012 Designed by My Blogger Tricks