Na Joseph Mihangwa.
MWAKA 1992, muda mfupi kabla nchi yetu haijaingia kikamilifu kwenye mfumo wa uchumi wa soko na siasa huria, Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), iliketi mjini Zanzibar na kurasimisha sera za mfumo huo huria chini ya kile kilichokuja kujulikana kama “Azimio la Zanzibar”.
Azimio hili, ambalo kwa sehemu kubwa lilizingatia sera na masharti ya taasisi mbili za ubepari na ubeberu wa kimataifa – Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), lilifungua milango kwa sera za nguvu ya soko kuongoza uchumi, na kwa serikali ya wananchi kujiondoa katika kupanga na kusimamia uchumi kwa ajili ya maendeleo ya watu wake ili kwamba kazi hiyo ifanywe na nguvu ya soko kupitia sekta binafsi.
Kwa wengi, Azimio la Zanzibar lilionekana (na mpaka sasa linaonekana) kama hatua ya kuuwa itikadi/sera ya Ujamaa na Kujitegemea, kama inavyofafanuliwa kwenye Azimio la Arusha, kama tutakavyoona baadaye katika makala haya.
Hata hivyo, CCM na serikali yake, inapinga dhana hii ya kuuawa kwa Azimio la Arusha wala Ujamaa; bali kwamba lilicholeta na kuingiza Azimio la Zanzibar, ni mazingira mapya ya kiuchumi na kijamii ambamo Ujamaa utaweza kutekelezwa, kama inavyofafanuliwa chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, ibara ya 9 kwamba:
“Lengo la Katiba hii ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.…. Kutokana na kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambayo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya Kijamaa kwa kuzingatia mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano”.
Sina hakika na Serikali ya watu wa Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba inakubaliana au la na matakwa ya ibara hii; kwani tangu enzi za Rais wa Serikali ya awamu ya kwanza ya Zanzibar, na mmoja wa waasisi wawili wa Muungano, hayati Abeid Amani Karume, ilitamkwa wazi kwamba, mwisho wa sera za itikadi ya Ujamaa na Azimio la Arusha ni kisiwa kidogo cha mpakani mwa Tanzania Bara na Zanzibar, Tunguu; kwa maana kwamba, Zanzibar haikutambua Azimio la Arusha wala Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Pengine ni kwa sababu hii kwamba, NEC ya CCM iliamua kuliuwa Azimio la Arusha huko huko Zanzibar ilikopigwa “stop” ili kuimarisha Muungano wa nchi hizi mbili, na pia kuimarisha Muungano wa vyama asisi vya TANU (Tanzania Bara) na ASP (Zanzibar), vilivyounda CCM mwaka 1977.
Nasema kuuawa kwa Azimio la Arusha kwa sababu, Katiba yetu (ibara ya 9) pamoja na mambo mengine, licha ya kutamka kwamba Serikali ya Muungano ihakikishe “utajiri wa nchi, unahifadhiwa na kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mwingine”; na kuhakikisha kwamba, “matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umasikini, ujinga na maradhi; na pia kwamba, “shughuli za Uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi kuwa katika mamlaka ya watu wachache binafsi”; laikini kinyume chake, yanayotokea na kutekelezwa nchini ni tofauti na mbali kwa vigezo vyote na matakwa hayo ya kiKatiba na Ujamaa kwa ujumla.
Pamoja na matakwa hayo wazi ya Katiba, leo ni Mtanzania yupi asiyejua au kuona jinsi utajiri wa nchi unavyoporwa (madini na wanyamapori hai), na jinsi unavyotumika kwa manufaa ya wachache ndani ya unyonyaji uliokithiri?
Ni mwananchi yupi asiyefahamu jinsi wananchi wengi wanavyozidi kuzama kwenye lindi la ujinga, maradhi na umasikini kuliko tulivyokuwa kabla ya uhuru? Ni mwananchi yupi asiyefahamu au kuona, jinsi shughuli za uchumi na utajiri wa nchi ulivyohodhiwa na kikundi kidogo cha “wateule” wachache, kwa manufaa binafsi ya wachache hao?
Yote haya ni kinyume cha Ujamaa, na ni ukiukaji wa Katiba pia.
Kama kweli Azimio la Arusha halikuuawa, kwa nini tuliowapa mamlaka ya kuongoza na kusimamia sera za uchumi wa nchi hii hawachukui hatua? Kwa Katiba yetu imegeuzwa pambo, kwa maana ya Sheria mama isiyo na nguvu; kwa nini tusiamini kwamba, matakwa ya Katiba hiyo ni danganya “toto” kwa wananchi na hatua fulani tu ya “funika kombe mwanaharamu apite”? Kama si hivyo, kwa nini hatuoni hatua zikichukuliwa kwa Katiba kukiukwa kiasi hicho?
Je, kuna mtu au kikundi cha watu kilicho juu ya Katiba ya nchi, kama si kwamba Katiba imetekwa nyara na kuhodhiwa na kikundi cha “wateule” wachache chenye kusimamia maslahi ya kitabaka?
Kutekwa kwa Katiba maana yake ni wananchi kuporwa demokrasia na chombo cha kuwasemea – Bunge. Ni kwa sababu hii hatushangai leo kuona Bunge limesaliti wananchi, limeacha kutumikia, sasa linataka kutumikiwa. Yote haya tumeyaona wakati wa Kikao cha Bunge la Bajeti kilichopita.
Chama kimesaliti uzalendo, utaifa?
Chimbuko la itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea ni wazo la Chama cha “Tanganyika African National Union” (TANU) mwaka 1962, ambapo wakati huu, chama hicho kilikuwa cha utaifa na uzalendo (nationalist) zaidi kuliko Chama cha siasa.
Kilikuwa na kiu kwa nchi kupata itikadi sahihi na makini kwa maendeleo, na kuliponya taifa hili majeraha na maovu yote ya ukoloni mkongwe kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.
Mwaka 1962, Rais wa kwanza wa Tanganyika huru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika kijitabu chake kidogo “Ujamaa”, alijadili kwa kirefu aina na misingi mbali mbali ya Ujamaa wa Kiafrika kwa kubainisha kuwa “Ujamaa ni IMANI” inayojengeka ndani ya uzalendo wa mwananchi.
Ndiyo kusema kwamba, bila uzalendo hakuna Ujamaa, na pale ambapo hapana uzalendo, hakuna uzalendo. Vivyo hivyo, tunaweza kusema kutetereka kwa Ujamaa nchini mwetu ni matokeo ya kutetereka kwa uzalendo, kama tutakavyoona baadaye katika makala haya.
Katika kijitabu hicho, Mwalimu aliandika, pamoja na maoni mengine, kwamba: “Sio ufanisi katika uzalishaji, wala kiwango cha utajiri nchini, unaozaa mamilionea; ni ugawaji usiozingatia haki na usawa kwa kile kinachozalishwa. Tofauti ya msingi kati ya jamii ya Kijamii na jamii ya kibepari sio namna utajiri unavyozalishwa, bali namna utajairi huo unavyogawanywa”.
Mahali pengine Mwalimu alisema: Ule usawa wa binadamu mbele ya Mungu, ambao ndo msingi wa dini kuu zote duniani, ndio msingi pia wa falsafa ya kisiasa ya Ujamaa….
Kwa hiyo, Ujamaa, ni matumizi ya msingi ya usawa wa binadamu katika mfumo wa jamii kijamii, kiuchumi na kisiasa.”
Hatimaye, mwaka 1967, NEC ya TANU iliyoketi mjini Arusha, Januari 26 – 29, ilifikia uamuzi kuwa Tanzania iongozwe kwa misingi ya Ujamaa kama itikadi ya Chama (TANU); uamuzi ambao uliridhiwa na Mkutano Mkuu wa Chama hicho siku chache baadaye, na kuchapishwa Februari 5, 1967 kama “Azimio la Arusha”.
Kwa Azimio hilo muhimu pengine muhimu kuliko maazimio mengine yaliyowahi kutolewa na TANU, chama hicho kilikuwa kinatangaza vita dhidi ya aina zote za uonevu, unyanyasaji na unyonyaji.
Madhumuni makubwa ya Azimio hilo yalikuwa ni matatu: Kwanza, ni kusimamia haki ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote; Pili, kuimarisha na kulinda uhuru wa nchi hii na wa watu wake, na kudumisha heshima ya kibinadamu na uhuru wao; Tatu, kuleta maendeleo ya kiuchumi haraka (kwa manufaa ya wananchi wote) na kujitegemea kwa Taifa.
Pamoja na Azimio la Arusha juu ya Ujamaa, TANU kiliweka “Maadili ya Uongozi” (The Leadership Code) mwaka 1971, kuzuia wenye madaraka ndani ya chama, serikali na mashirika ya umma kujilimbikizia mali kwa njia ya kumiliki hisa au kuteuliwa kuwa wakurugenzi katika makampuni binafsi; kupokea zaidi ya mshahara mmoja, na kumiliki nyumba za kupangisha.
Zaidi ya hilo, TANU kilijiwekea mwongozo (Guideline), uliotaka watendaji wakuu serikalini na Chama, na wananchi kwa ujumla, kuelewa maana halisi ya shughuli za Kijamaa na kidemokrasia, kudhihirisha kuwa kilichokuwa kimedhamiria kupigania uhuru kwa Tanzania na Watanzania, Afrika pamoja na ujenzi na utetezi wa uchumi wa Taifa.
Yote haya yaliwezekana kutokana na kuendelea kukua kwa uelewa juu ya umasikini wa nchi, unyonge na utegemezi. Na hili liliwekwa wazi na TANU katika Azimio la Arusha (uk 4) kwamba:
“Tumeonewa kiasi cha kutosha; tumenyonywa (tumetumikishwa) kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliofanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka kufanya mapinduzi ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na tusipuuzwe tena”.
Miaka 10 ya Azimio (1977) ilikuwa na mengi kuweza kubatizwa kuitwa “Sherehe za kisiasa” (Political Festival) Kwanza ilikuwa ni miaka 10 ya kujipima kiutekelezaji; pili ni kuungana kwa Vyama vya TANU na ASP kuunda “Chama cha Mapinduzi” – CCM; na tatu, kuanzishwa kwa Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano.
Katika hotuba yake (soma kijitabu – miaka 10 ya Azimio la Arusha), Mwalimu alisema, japo nchi ilikuwa haijawa ya Kijamaa, lakini unyonyaji ulikuwa umelegea na kubadilika, na kwamba ingetuchukua miaka zaidi ya 30 iliyotarajiwa (hadi 1997) kuwa Wajamaa kamili.
Mwalimu aliyataja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kumalizika kwa matabaka na ubaguzi ulioambatana nayo; huduma za afya na elimu kwa wote, na katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji na viwanda vidogo vidogo.
Kero za Ujamaa kwa Wazanzibari
Kama tulivyoona hapo juu, Ujamaa kwa misingi ya Azimio la Arusha ulikusudia kufanya mapinduzi dhidi ya uonevu, unyonyaji na kupuuzwa kwa wazalendo nchini na tabaka la wachache. Kwa nini, na kwa misingi gani Rais Karume alipiga marufuku Ujamaa na Azimio la Arusha Visiwani?
Je, kuungana kwa Vyama vya TANU na Afro-Shirazi (ASP) kuunda CCM kulihalalisha Ujamaa na Azimio la Arusha kutumika Zanzibar?
Kwa kutangaza Azimio la Arusha, TANU kilikuwa kimejitambua kama Chama cha Mapinduzi dhidi ya maovu ya kijamii, kiuchumi na kisiasa nchini, kama ambavyo ASP tayari kilikuwa kimejitambua hivyo mapema dhidi ya maovu hayo, kufuatia Mapinduzi ya wamwagaji damu Visiwani, Januari 12, 1964.
Tatizo hapa lilikuwa ni la kimitizamo, kwamba, ingawa vyama vyote vilikuwa vilijitambua kwa shughuli za kimapinduzi dhidi ya maovu niliyoyataja, lakini kimsingi, Chama na Serikali ya Mapinduzi yaliyotokana na matumizi ya silaha na umwagaji damu (ASP), ni tofauti na Chama na Serikali (TANU) inayoendesha Mapinduzi kwa vikao mezani (Azimio). Hivi vyote vina utamaduni tofauti na utekelezaji kwa mazingira tofauti. Na ili viweze kufanya kazi kwa malengo ya pamoja, kunahitaji ndoa thabiti, kwa kila kimoja kukubali kupoteza mengi.
Kwa mfano, chama kilichoingia madarakani kwa silaha na umwagaji damu (kama ASP) siku zote ni cha ki-imla na huendesha mambo kwa matumizi ya nguvu na udikteta, tofauti na Chama kilichoingia madarakani kwa nguvu ya hoja (TANAU) ambacho huendesha mambo kwa kuelezea na kushawishi.
Tofauti hizi zinajikita pia katika namna uhuru wa nchi hizi mbili ulivyopatikana. Kwa Tanzania Bara, ilikuwa “mtu mmoja kura moja”, lakini kwa Zanzibar, ilikuwa “mtu mmoja panga moja”.
Kwa hiyo, Rais Karume alikuwa sahihi kupiga stopu kutumika kwa mapinduzi ya Ujamaa na Azimio la Arusha Visiwani. Isitoshe Vyama vya Siasa (TANU na ASP) havikuwa jambo la kikatiba, wala la Muungano, kuweza kushurutisha Zanzibari ilikubali; na vivyo hivyo mpaka sasa.
TANU/ASP adui wa Ujamaa?
Hali hiyo ya kuwa na Vyama viwili vya Kimapinduzi (TANU/ASP) vyenye tamaduni na itikadi za kimapinduzi tofauti na mazingira ya utendaji kazi yasiyoshabihiana, ilikuwa kero na adha kubwa kwa uendeshaji wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano yenye mfumo wa demokrasia ya Chama kimoja cha siasa.
Kutoshabihiana huko kwa mitizamo ya kimapinduzi, kati ya TANU na ASP kulifanya pendekezo la kwanza la kuunganisha TANU na ASP mwaka 1975, likataliwe na Rais wa Serikali ya awamu ya pili Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, kwa madai kwamba alihitaji muda wa kutosha kufikiria.
Maridhiano ya kuunganisha vyama hivyo yalipofikiwa Oktoba, 6, bado yalikumbana na kazi ngumu ya kupata jina lenye kukubalika kwa pande zote mbili, kila upande ukitaka kuwa na jina linalowakilisha mtizamo wake wa kimapinduzi.
Wakati TANU ilisisitiza kutotaka kupoteza kumbukumbu ya tarehe ya kuasisiwa kwa Azimio lake la kimapinduzi (Azimio la Arusha) Februari 5, 1967, ASP nacho hakikutaka kupoteza jina “Mapinduzi” (na hadhi ya Baraza la Mapinduzi) yaliyong’oa udhalimu wa kikoloni Visiwani Zanzibar kwa umwagaji damu.
Ili kuleta mwafaka, ilikubaliwa kuwa, Februari 5 (1977), ambayo ni siku ya kuzaliwa kwa Azimio la Arusha, iwe ndiyo siku ya Muungano wa TANU na ASP; na kwamba jina la Chama kipya liwe “Chama cha Mapinduzi” kuwakilisha dhana ya “Mapinduzi” ya vyama vinavyoungana, ingawaje kwa mitizamo na mazingira tofauti ya “mapinduzi”.
Ni kwa sababu hii Azimio la Arusha lingali na mtizamo hasi kwa upande wa CCM Visiwani kwa misingi ya “Mapinduzi” ya Zanzibar, lakini lina mtizamo chanya Bara kwa misingi ya Mapinduzi ya wanyonge Tanzania Bara.
Ni kwa sababu hii pia kwamba, licha ya misingi ya Azimio la Arusha kuwekwa bayana kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano (ibara ya 9), kama nilivyoelezea mwanzo, utekelezaji wake ni wa kuparanganya kutokana na ukweli kwamba, Katiba ya Muungano inashinikiza Zanzibar itekeleze Mapinduzi “laini” ya Azimio la Arusha katika mazingira yake, wakati Zanzibar inashabikia Mapinduzi ya “kiharakati” yaliyopatikana kwa umwagaji damu.
Lakini pamoja na ukinzani huu wa kimtizamo juu ya “Mapinduzi” kati ya Bara na Visiwani, kwa nini Ujamaa umeshindwa kuleta ukombozi uliotarajiwa nchini; japo kwa Tanzania Bara?
Credit to: RAIA MWEMA
No comments:
Post a Comment