Study in South Africa: (www.southafricauniversities.blogspot.com) or Uganda: (www.ugandauniversities.blogspot.com)

Pages

Friday, October 11, 2013

Mzimu wa Azimio la Arusha wafufuliwa: Wasomi wanasiasa wakutana kulirudisha

HALI ya kisiasa haijatulia nchini, kivuli cha Azimio la Arusha lililotetewa na Mwalimu Julius Nyerere hadi kifo chake, kimeanza kuzonga si tu wanasiasa wakubwa, akiwamo rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyejitetea hivi karibuni kutoliua na mbadala wake kuwa Azimio la Zanzibar, sasa wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamecharuka, wanakutana kuchambua na kusisitiza umuhimu wa azimio hilo, Raia Mwema, imethibitishiwa.

Wasomi hao wameibuka kutetea azimio hilo katika wakati ambao ufisadi umeligubika Taifa, hali ya maisha ikiwa ngumu miongoni mwa watu masikini nchini na wakati huo huo, viongozi wa kisiasa wakifikiria kuongeza gharama za uendeshaji siasa nchini kwa kuongeza idadi ya majimbo ya uchaguzi.

Kwa upande mwingine, wasomi hao pia wanaibuka katika wakati ambao umma ukisubiri kesi nyingi zaidi za ufisadi unaohusu vigogo kufikishwa mahakamani, kama ambavyo ilivyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete katika kipindi maalumu cha “Maswali kwa Rais” ambako alisema kuna kesi tano kubwa zinazohusu vigogo zitakazofikishwa mahakamani, lakini hilo halijatokea miezi kadhaa sasa.

Wanazuoni na wanadiplomasia hao mashuhuri Afrika na duniani  wamepanga kujadili azimio hilo wakati wa tamasha la Wiki ya Kitaaluma ya Mwalimu Nyerere, linaloratibiwa na Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, ambacho Mwenyekiti wake ni Profesa Issa Shivji. Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Nkrumah, UDSM, wiki ijayo.

Azimio la Arusha, lililoasisiwa na Mwalimu Nyerere mkoani Arusha, mwaka 1967 liliweka misingi ya uongozi Tanzania, yakiwamo maadili ya viongozi. Katika azimio hilo, ilielekezwa namna kiongozi wa umma anavyopaswa kuishi kimaadili, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maslahi ya umma yanalindwa.

Katika kongamano hilo, wasomi hao wamejipanga kutafakari na hatimaye kuibua jawabu juu ya nini cha kufanya baada ya kuvurunda kwa muda mrefu kutokana na kutelekezwa kwa Azimio la Arusha. Inaamika na wasomi hao kuwa Azimio la Arusha bado ni jibu la kilio cha Watanzania wengi masikini katika kudhibiti viongozi na matumizi bora ya rasimali za nchi.

Magwiji wa taaluma mbalimbali, wakiwamo maprofesa zaidi ya 15 wa ndani na nje ya nchi, wanatarajiwa kushiriki kuchambua faida za Azimio la Arusha kama ambavyo lilitetewa na Mwalimu Nyerere. Miongoni mwa vinara wa kongamano hilo ni Profesa Shivji mwenyewe, mtoto wa aliyekuwa rais wa kwanza wa Ghana Dk. Nkwame Nkrumah Bi. Samia Nkrumah na Profesa Samir Amin.

Wengine ni Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekeza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Rhodes cha Afrika Kusini, Dk. Saleem Badat, Mhadhiri wa UDSM, Bashiru Ally; Profesa Mugyabuso Mulokozi wa UDSM, Profesa Kofi Anyidoho na Prof. Zenebeworke Tadesse wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa.

Orodha ya vinara wengine ni Profesa Sam Moyo, wa Africa Institute of Agrarian Studies, Harare, Zimbabwe; Profesa F. Senkoro, Profesa Utsa Patnaik kutoka India na Dk. Said Adejumobi, Dk. Ebrima Sall. Mwanadiplomasia mahiri, Dk. Salim Ahmed Salim anatarajiwa kuongoza moja ya vikao vya kongamano katika siku ambayo mgeni rasmi atakuwa Dk. Marcelino dos Santos, wakati Profesa Shivji akiongoza kikao katika kuchambua fikra za Mwalimu katika mada mahsusi iliyopachikwa kichwa “Fikiri na Mwalimu.”

Dk. Salim aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), anatarajiwa kuongoza kikao hicho Aprili 13, mwaka huu, kuhusu ukombozi wa Afrika na mtazamo na juhudi za Mwalimu Nyerere.

Katika kongamano hilo miongoni mwa nukuu za Mwalimu Nyerere zitakazong’arisha ukumbi wa Nkrumah, UDSM ni ile inayoeleza:  “Watu wanaoogopa mapinduzi ni wanyonyaji; na wote wanaoogopa mabadiliko ni wanyonyaji tu. Watu walioshiba ndio wanaoogopa mabadiliko, kwa sababu mabadiliko yale yatawatia mashaka.

“Lakini mnyonge lazima atake mapinduzi; mnyonge hawezi kutaka mambo yaende hivi hivi tu na huku ananyonywa. Mnyonge hawezi kutaka hali hiyo; wanaoshikilia hali hiyo ni wale walioshiba, si wanyonge.” Nukuu hii ni ya mwaka 1973, katika kitabu cha Ujamaa ni Imani: Moyo Kabla ya Silaha.

Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. Mukandala ambaye pia ataongoza vikao kadhaa, anatarajiwa kutoa ujumbe mahsusi utakaolenga kusisitiza masuala ya utafiti na majadiliano kuhusu changamoto za kisiasa na uchumi katika maendeleo ya Tanzania na Afrika kwa ujumla, ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere.

Katika kile kinachoweza kuelezwa kuwa kivuli cha Azimio la Arusha kimekuwa kikimzonga hata rais mstaafu Mwinyi, Machi 18, mwaka huu, alizungumzia azimio hilo katika tafsiri inayodhihirisha kujivua lawama. Katika kuzungumzia azimio hilo ikiwa ni takriban miaka 15 tangu astaafu urais, Mwinyi alisema Azimio la Arusha halikufutwa bali lilizimwa na baadhi ya viongozi aliowaita si wacha Mungu, ambao kwa mtazamo wake ndio chanzo kikuu cha kuuzwa kwa mashirika ya umma.

Alikiri uzuri wa Azimio hilo, lakini kwa upande mwingine akisema ili litekelezwe kwa ubora ilihitaji viongozi wa makanisa na misikiti “kufinyanga” watu wao wamche Mungu ili kulitekeleza.

Katika maelezo yake hayo aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa Benki ya Mkombozi iliyoanzishwa na Kanisa Katoliki Tanzania, Mwinyi alisema baadhi ya viongozi sasa wanalilia Azimio hilo baada ya kuona mambo yanazidi kuvurugika, lakini akisisitiza kuwa ni vema ikafahamika kuwa halikufutwa bali lilizimwa na baadhi ya mambo.

“Azimio la Arusha halikufutwa, wala lile la Zanzibar halikufuta la Arusha, lilizimwa na baadhi ya mambo ambayo hayakwenda vizuri, hakuna siasa nzuri na bora kwa Watanzania kama ya Ujamaa, ile ambayo ililetwa na mwalimu Nyerere, lakini inaelekea kwamba nia hiyo ilitangulia uwezo wa Watanzania,” alisema Mwinyi.

Mwinyi alisema kwa mfano wakati ule kulikuwa na mashirika ya umma yapatayo 400, lakini yalikuwa magamba tu, ‘yamegunguliwa (yametafunwa)’ kama mchwa anavyotafuna mti wa msonobari, huku kwa nje ukibaki mzuri kumbe kwa ndani hauna kitu.

“Viongozi hao wamegungua mashirika hayo kama kunde inavyotafunwa na wadudu, nje nzima kumbe ndani gamba tupu … watu bado walikuwa hawajapatikana, ndiyo maana mashirika yaliuzwa baada ya kuonekana ni mzigo kwa Taifa,” alisema.

Alisema wengi walioendesha mashirika hayo hawakumwogopa Mungu na kwamba katika uongozi uliopo, ipo haja ya kuomba taasisi za dini kufinyanga vijana wanaomwogopa Mungu ndipo wapewe dhamana.

Credit to: http://www.raiamwema.co.tz/mzimu-wa-azimio-la-arusha-wafufuliwa

No comments:

Post a Comment

© 2012 Designed by My Blogger Tricks