Na Privatus Karugendo.
Ndugu mzomaji, unaposoma makala hii Tamasha la Wiki ya Kitaaluma ya Mwalimu Nyerere litakuwa linaendelea Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Tamasha hili lilianza juzi, Aprili 12, na litaendelea hadi Alhamisi, Aprili 15.
Mada nyingi zitawasilishwa na wageni mashuhuri kama vile binti wa marehemu Nkrumah, Samia Nkrumah, Profesa. Samir Amin, Kamaradi Marcelino Dos Santos na wengine kadhaa.
Tofauti kidogo na mwaka jana, tamasha la mwaka huu linajadili Azimio la Arusha. Bahati mbaya wale waliojaribu kulifukia Azimio la Arusha waliusahau kabisa msemo kwamba “Kilichoandikwa Kimeandikwa”. Hata kama wangefanikiwa kuvichoma vitabu vyote vya Azimio la Arusha, bado kilichoandikwa kingebakia mioyoni mwa watu.
Bahati mbaya tena hawakukumbuka kuandika kwamba wamefuta na kulizika Azimio la Arusha, hivyo kulifuta Azimio la Arusha si kitu kilichoandikwa! Mbaya zaidi ni kwamba hata na mifumo yao iliyofuata baada ya kulifuta Azimio la Arusha, haikuandikwa! Walilifuata Azimio la Arusha tukabaki na Ombwe!
Azimio la Arusha lilipinga mfumo wa Ubepari na kupendekeza mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea. Tunakumbuka sote misemo ya Ujamaa ni utu na Ubepari ni unyama. Na kusema kweli, hata ukiachia mbali Azimio la Arusha, ukweli unabaki pale pale kwamba Ubepari una maadili machafu.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema Ubepari ni unyama. Wengine walielewa na wengine hawakuelewa kabisa. Lakini hata na wale walioelewa wakati ule, sasa hivi wanajifanya kutoelewa tena. Hakuna anayehoji wala kujadili tena juu ya msamiati huo.
Wale ambao ndio wangehoji, hivi sasa, wamezama kwenye biashara halali na haramu ya kutafuta fedha; maana walichelewa! Hata hivyo, ukweli unabaki palepale kwamba Ubepari ni unyama - ni mfumo unaojali pesa na si pesa inavyopatikana.
Ukiwa na klabu ya usiku ambako wasichana wanatembea uchi kufurahisha wateja, kwa mtazamo wa kibepari, hakuna shida; maana biashara hiyo inazalisha kodi ya serikali!
Kwenye mji fulani wa Nchi Zilizoendelea na zinazoukumbatia mfumo wa Ubepari, nilikuta tangazo la ajabu katika mashine ya kuuza sigara. Hii ni mashine ambayo unatakiwa uweke pesa na ikupe pakiti ya sigara.
Tangazo linasomeka hivi: “Sheria zetu zinatukataza kumuuzia sigara mtu yeyote aliye chini ya umri wa miaka 16”. Mimi kilichoniogopesha si tangazo wala si sigara. Nilishtuka jinsi teknolojia ilivyopanuka. Yaani mashine kuweza kupima umri wa mnunuaji?
Nilishangaa na nikaanza kuuliza kwa watu mbalimbali kama teknolojia imefikia kiwango hicho. Wapi? Jamaa wote niliowauliza waliniambia haipimi umri wanachotaka ni pesa. Hata kama una miaka miwili ukiweka pesa unapata pakiti ya sigara. Sijui tangazo ni la nini.
Zipo mashine nyingi za kuuza vileo vya kila aina na kila kona. Hazipimi umri. Unachotakiwa uweke pesa yako upate kilevi. Lakini tangazo lipo: Sheria zinakataza umri mdogo kuuziwa kilevi!
Mfumo unaojali pesa bila kujali zitakavyopatikana ni hatari. Hata kama ni kwa kuhatarisha afya za binadamu, katika ubepari hakuna ubaya wowote.
Leo hii vyakula tunavyokula ni vya ajabu kabisa. Mbegu zinawekwa kemikali za ajabu, zinakuzwa kwa siku chache na lengo kuu ni faida haraka kwa mabepari.
Dawa za magonjwa ya binadamu zina faida ya kubwa sana. Nyingi ya dawa hizo hazitengenezwi kukutibu au angalau kukuwekea kinga ya muda mrefu; bali zinakujengea utegemezi mbaya sana. Zinakufanya uwe mtumwa wa dawa kwani zinapunguza kinga ya asili ya mwili taratibu. Unatengenezwa kuwa soko lao milele!
Historia ya utabibu inatuambia kwamba kabla ya chanjo kugunduliwa miaka ya 1700, mwili wa binadamu ulikuwa unaweza kabisa kupambana na magonjwa mbalimbali. Tangu kugunduliwa kwa chanjo, matatizo yamezidi kuwa mengi mno.
Miili ya binadamu inafanyiwa majaribio ya dawa hatari za sumu. Lakini nieleweke kwamba hata mabadiliko ya dunia na shughuli za binadamu ambazo pia hazijali athari za mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa duniani, zimefanya magonjwa kuongezeka.
Sasa hivi magonjwa ya kansa yameongezeka kwa kasi duniani sababu mojawapo ikiwa ni mtindo wa maisha ikiwemo ulaji wa vyakula na unywaji wa vinywaji ambavyo ni hatari kwa miili ya binadamu.
Siku za nyuma tatizo la saratani lilikuwa si kubwa sana katika nchi za Dunia ya Tatu. Sasa hivi limeongezeka kwa kasi sana na tunaambiwa kwamba ifikapo mwaka 2020 asilimia 60 ya wagonjwa wa kansa watatoka Afrika. Hali hii inatisha. Ukiongeza malaria, kipindupindu, ukimwi na magonjwa mengine ya umasikini, kuna hatari Afrika itakwisha!
Unatakiwa uelewe wazi kwamba kuna dawa zinazotengenezwa na mabepari kukuza biashara ya kampuni za dawa za nchi za Magharibi.
Leo hii madaktari, wafamasia na watafiti wengi wa magonjwa wanasomeshwa na kampuni za dawa za nchi za Magharibi si kwa lengo la kutafuta suluhisho la matatizo ya binadamu, bali kuja kusaidia kutangaza soko lao la dawa.
Hawataki kabisa kusikia utafiti wa dawa mbadala za jadi. Wakisikia watazipinga mpaka mwisho. Watatumia wanasiasa, wataalamu wa fani zote na yeyote anayeweza kutumika kwa masilahi yao na kwa vile nchi za Dunia ya Tatu zimefungwa kabisa kufikiri, basi, wataimba na kutukuza dawa za Magharibi na kuacha hata kusikiliza chochote kuhusu dawa za asili ambazo nazo zina umuhimu wa kipekee kabisa katika miili yetu.
Leo ukimwi umekuwa sekta nyeti kweli na dili la nguvu kwa kampuni za dawa za Magharibi. Ndio maana makuhani wa Ubepari wanakataa nchi changa zisijiingize katika kutengeneza hizo dawa. Wanajua nchi kama India, Brazil na China ambako gharama za uzalishaji ni chini, wakianza kuzalisha, basi, bei zitashuka na faida zao zitapungua. Wanalinda kweli zisizalishwe katika nchi hizo. Wanatumia hilo dubwasha lao waliloanzisha linaloitwa Shirika la Biashara Duniani (WTO).
Ile migahawa ambayo sasa inashamiri kwa kasi Jijini Dar-es-Salaam kama vile McDonalds, Nandos, Steers, KFC na mingineyo ambayo tunaaminishwa ni maendeleo, ni ya hatari. Vyakula vinavyopikwa humo; hasa kuku ndio hao waliokuzwa kwa wiki mbili kwa kutumia vimiminika vya kikemikali ambavyo si salama kwa mwili wa binadamu.
Yote hayo ni katika kukuza biashara ya mabepari. Haijalishi afya ya mlaji. Pesa kwanza halafu wanajua magonjwa yatakufuata baadaye na utanunua dawa kwao tena. Chakula kinazalisha ugonjwa na ugonjwa utazalisha pesa kwa kuuza dawa zao.
Biashara ya silaha nayo usiseme. Inaendelea kwa kasi ya ajabu. Mbaya zaidi silaha hizo zinapelekwa nchi zenye matatizo ya kivita ili watu waendelee kuchinjana. Wanakuwa kwanza na ajenda ya kutoa msaada wa kijeshi kwa nchi changa.
Watakuambia wanakusaidia kufundisha jeshi lako, na kwa vile tumeshaapa kutofikiri tunakubali haraka bila kuuliza kwa nini tunapewa msaada huo? Takwimu zinaonyesha kwamba misaada na mauzo ya silaha za kijeshi toka Marekani kuja Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara, imeongezeka kwa kasi sana.
Kwa mfano, fedha kwa ajili ya msaada wa kijeshi iliongezeka toka dola milioni 12 mwaka 2000 hadi kufikia dola milioni 24 mwaka 2006. Hii ni mara mbili ya kiwango cha mwaka 2000.
Misaada hii ni ya kupumbaza Waafrika ili kesho ukiwa na mahitaji ya silaha ukimbilie kwao uzidi kuwaongezea fedha, na huku tukizidi kuuana.
Wakati tunachinjana kwa hizo silaha, mabepari wa dunia watakuwa wanakunywa mvinyo na kusherehekea; huku wakiiba rasilimali zetu.
Kuna watu wanafikiri kwamba vita nyingi katika nchi za Kiafrika zinashindwa kwisha. Si kweli. Ukweli ni kwamba hawa mabepari wakishagundua kwamba kukiwa na vita kuna faida kuliko amani, basi, watataka hiyo vita iendelee. Vita itaendelea mpaka pale ambapo itaonekana kwamba hailipi kuendelea kupigana au pale wanapoona kwamba wameshapata kibaraka atakayeshirikiana nao kupora wanachotaka.
Haya ndiyo yaliyotokea Angola wakati wa marehemu Jonas Savimbi. Baada ya kuiba almasi za Uhambo akishirikiana na Marekani kwa miaka zaidi ya 20 na kuua Waangola kwa maelfu, wakaamua sasa kumuua kwa vile wizi wa almasi na mafuta ungeweza kuendelea hata Savimbi asipokuwepo.
Hawa jamaa (mabepari) ndicho wanachofanya, na kwa vile wamegundua nasi tunawaamini sana watakuja na vizawadi kama wanavyotupa sasa hivi ili kuendelea kutumaliza.
Wakishindwa kutushawishi wanaanzisha vita wakishirikiana na baadhi ya Waafrika wanaokubali kuhadaiwa na vifedha na kuchinja ndugu zao kibao.
Wakati Waafrika wanaendelea kumalizana, wao wanaendelea kupora walichofuata.
Zamani wakati tunasoma historia shule za msingi na sekondari, tulifika mahali tukaanza kuwalaumu kina Chifu Mangungo wa Msovero na Lobengula wa Mashonaland kwa kukubali kulaghaiwa na Wazungu. Lakini je, kuna tofauti yoyote na sasa wanavyolaghaiwa viongozi wetu wanaoitwa wasomi kwa lugha za misaada, uwekezaji na misamiati mingine?
Ni njia za ulaghai na misamiati tu imebadilishwa. Misamiati ya kibepari imekuwa tofauti na inaficha ulaghai wa moja kwa moja siku hizi lakini ukiwa na akili zako utagundua hakuna tofauti.
Ni kama watu wengine wanavyofikiri kwamba kuna tofauti ya mifumo ya mwanzo ya ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo na kinachoitwa sasa utandawazi. Mambo ni yale yale, labda mbinu tu ndizo zimebadilika kutokana na maendeleo na hasa teknolojia ya habari na mawasiliano.
Ukikumbuka jinsi Kwame Nkrumah alivyouelezea Ubeberu, basi, haitakiwi uyatofautishe hayo mambo. Nkrumah alisema Ubeberu ni kama kinyonga, hubadilika rangi kutokana na mazingira. Suala ni kwamba (Ubeberu) unaendelea
kuwa kinyonga yule yule.
Ni lazima tuwe macho na kujali maadili yetu, tamaduni na taratibu zetu. Tamaduni na mitindo yetu ya maisha ni mizuri tu, vyakula ndio usiseme. Ukienda kula McDonalds unatafuta matatizo ya bure kabisa! Dawa za asili ni kiboko ni kwa vile tu tumeamua kuziacha na hazitafitiwi.
Hebu fikiria, Wazungu wanawatuma wanafunzi wao kuja Afrika kuzitafiti dawa hizo. Wanafanya hivyo kwa kuwa wanajua baadhi zinatibu kweli kweli.
Hofu ni kwamba watazipora zote na kuzimaliza. Tulinde chetu kidogo kilichobaki, tusiachie kila kitu angalau tubaki na cha kusema hiki ni chetu.
Azimio la Arusha, lilipendekeza mfumo mbadala. Huu ni mfumo wetu, ni historia yetu! Kwa vyovyote vile, kwa kuwa Azimio la Arusha limeandikwa, halikwepeki. Tukishindwa kulitekeleza sisi, litatekelezwa na vizazi vijavyo. Ubepari hauwezi kudumu maana una maadili machafu!
Credit to: http://www.raiamwema.co.tz/kilichoandikwa-kimeandikwa-azimio-la-arusha-halitakufa
No comments:
Post a Comment