Na Deogratius Temba.
HATUWEZI kuishi bila Historia, Chama cha Mapinduzi (CCM), chama kilichopigania uhuru wa taifa hili kwa kushirikiana na wananchi wazalendo ambao hawakuwa na chama, kimeshiriki kwa kiasi kikubwa kuzika tunu za maadili, uzalendo na miiko ya utaifa wetu.
Taifa limekuwa pori la wanyang’anyi, kila mtu ni mporaji, tumeunda vyombo vya kutudhibiti sisi wenyewe (wezi), lakini vinatumia fedha za walipa kodi bila kutenda kazi, vyombo hivyo ni kama Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Tume ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kadhalika.
Vyombo vimeundwa lakini havijawahi kuwakamata wezi wa rasilimali zetu ambao waliingia madarakani wakiwa masikini wakatoka matajiri wa kutupwa.
Wanataka kutuambia kuwa wananchi ni vipofu? Ni kwanini watumie fedha zetu, hawatendi haki? Mzee wa vijisenti hakuonekana? Kuna tatizo kubwa katika taifa hili na hili ni la kihistoria.
Serikalini hakuna wa kumyoonyeshea mwingine kidole, CCM kimeshiriki kulizika Azimio la Arusha lililozaliwa mwaka 1967.
Kwa kuangalia suala la maadili na uzalendo kwa kipindi hiki tunaadhimisha miaka 50 ya uhuru; historia yetu ya nusu karne tunaweza tukaigawa kwa vipindi viwili: miaka 25 ya mwanzo (1961-1985) ambayo tunaweza tukaiita enzi ya kizalendo na miaka 25 iliyofuata (1986-2005) ambayo tunaweza tukaibatiza kama enzi ya uliberali-mamboleo.
Kilele cha enzi ya kizalendo bila shaka ni miaka 10 ya Azimio la Arusha, yaani, 1967 hadi 1977. Na kilele cha enzi ya uliberali-mamboleo ni miaka 10 ya utawala wa Benjamini Mkapa, 1995 hadi 2005.
Kama Hayati Mwalimu Julius Nyerere ni muasisi wa uzalendo nchini basi Benjamin Mkapa ni muasisi wa uliberali-mamboleo, mara nyingine huitwa enzi ya utandawazi. Vipindi vingine vya katikati ni vipindi vya mpito.
Baada ya 1977, na hasa baada ya vita vya Uganda mnamo mwaka wa 1979, uchumi wetu na hata siasa zetu zikaingia kwenye kipindi kigumu cha zahama (crisis).
Miaka mitano ya mwisho ya Mwalimu ilikuwa ya misukosuko kwa sababu mbalimbali za ndani na nje. Pamoja na sera za kimaendeleo wakati wa enzi ya Mwalimu, ukweli ni kwamba hatukufanikiwa kujikomboa kutokana na uchumi wa kibepari wa kimataifa, yaani ubeberu.
Tukaendelea kuwa na uchumi tegemezi. Katika ujenzi wa mfumo wa kijamaa makosa yalifanyika, mengine Mwalimu mwenyewe alikiri katika hotuba yake ya miaka kumi ya Azimio.
Ukweli ni kwamba badala ya kupanua demokrasia, madaraka mikoani yakapeleka utawala wa kirasimu karibu zaidi na wananchi; yakawa ‘madaraka mikononi’ badala ya ‘madaraka mikoani.
Matokeo yake ni umasikini
Kupotea kwa uzalendo na utu kumeongeza tabaka kati ya walio nacho na wasio nacho, masikini wameongezeka. Kati ya 2001 na 2007, idadi ya maskini, yaani wenye kipato chini ya dola 2 za Marekani, imeongezeka kuwa watu milioni 4.5. Ajira ni finyu. Karibu robo tatu ya wananchi hutegemea kilimo lakini kilimo huchangia robo tu ya pato la taifa.
Mfumo wa uchumi unaua ajira
Ajira katika sekta ya viwanda ni chini ya watu laki moja na haijaongezeka kati ya 2001 na 2007. Lakini ajira katika sekta isiyorasmi - yaani wachuuzi na wamachinga - imeongezeka kwa asilimia zaidi ya 90. Yaani wanaotegemea sekta isiyo rasmi, ni mara 17 ya ajira rasmi katika sekta ya viwanda.
Ajira ya akinamama wafanyao kazi majumbani kwa watu imeongezeka kwa asilimia 33. Hayo ni dalili za ugonjwa wa uchumi; si jambo la kujivunia.
Uwekezaji kutoka nje
Uwekezaji, ambao tunaambiwa, ni gurudumu la maendeleo umekua. Wastani wa uwekezaji kutoka nchi za nje kila mwaka kati ya 1997 na 2009 ni dola za Marekani milioni 439 lakini zaidi ya asilimia 95 ni katika sekta ya madini, sekta ambayo unachimba tu utajiri wa nchi na kusafirisha nje bila kuchangia katika kuendeleza uchumi wa ndani.
Kwa mfano, mchango wa madini kwa mauzo ya nje ni asilimia 39, lakini machango wa sekta ya madini kwa pato la taifa ni chini ya asilimia 3!
Mbaya zaidi uwekezaji wa dola milioni 439 kila mwaka umezaa ajira ya watu elfu 7,000, yaani ajira katika kazi za nyumbani ni mara kumi ya ajira migodini. Wakati huo huo wanaoingia katika soko ya ajira kila mwaka ni zaidi ya laki nane.
Sifa hizi nilizotaja ni sifa si tu ya uchumi tegemezi, kama alivyoainisha Mwalimu, lakini ni uchumi uchwara, kwa maana ya kwamba uchumi usioendelevu, uchumi usio na matumaini ya kuwaletea maendeleo walio wengi.
Huu ni uchumi wa kitabaka, unatugawa na hakuna uzalendo ndani yake kwa sababu umejaa majivuno, mwenye mali anaongeza na kumpora asiye nazo.
Kufa kwa azimio la Arusha na kupotea kwa tunu za maadili kumetufikisha hapa.
Credit to: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=33170
No comments:
Post a Comment