Study in South Africa: (www.southafricauniversities.blogspot.com) or Uganda: (www.ugandauniversities.blogspot.com)

Pages

Monday, October 14, 2013

Azimio la Arusha lilikufa na kilimo vijijini

Na Zitto Kabwe.

“Tusipoangalia tutakuja gundua kuwa wakaaji wa mijini nao ni wanyonyaji wa wakulima,” hili ni moja ya maonyo yaliyotolewa na Azimio la Arusha. Tunapomkumbuka Mwalimu Julius Nyerere hili ni jambo linalorejea sana kichwani mwangu.

Azimio la Arusha lilisisitiza sana tusisahau nafasi ya kilimo katika maelendeleo ya watu. Azimio lilitahadharisha kwamba mikopo mingi inayochukuliwa italipwa na wakulima kupitia mazao tunayouza nje ili kupata fedha za kigeni. Mara kadhaa Azimio lilisema ‘tusisahau jambo hili’ kwa maana ya nafasi ya kilimo. 

Tunapofanya kumbukizi la Mwalimu Nyerere nipo kwenye ziara ya chama changu cha siasa mkoani Tabora, Katavi na Kigoma. Ninazunguka kwenye vijiji vingi kuzungumza na wananchi kuhusu mabadiliko ya kisiasa na (mabadiliko ya kiuchumi?), umuhimu wa demokrasia ya vyama vingi. Pia kuzungumza na wananchi kuhusu Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika ziara hii jambo la dhahiri kabisa linaonekana ni kwamba licha ya uduni wa maendeleo ya nchi kiujumla, bado vijijini wananchi wanaishi katika hali duni zaidi kuliko watu wa mijini.

Huduma za kijamii ni za hovyo na hazilingani kabisa na umri wa Taifa letu tangu tupate uhuru. Kuna baadhi ya vijiji wananchi bado wanakunywa maji kwa kuchangia na mifugo yao.

Vijiji nilivyopiga vinalima mazao kama mahindi, mpunga na tumbaku. Ukilinganisha uzalishaji wao na hali zao unaona kabisa kuna jambo linahitaji maelezo.

Tumbaku ni zao la kwanza kuingia fedha za kigeni nchini katika kinachoitwa mazao asili. Mwaka 2012 tumbaku iliingiza dola za Marekani 350 milioni ikifuatiwa na kahawa. Hivyo ungetarajia kuona maisha ya wananchi hawa wanaolima tumbaku yangekuwa na ahueni. La hasha! 

Unyonyaji dhidi ya wakulima ni mkubwa na unatisha. Mfumo wa biashara ya tumbaku umejengwa katika misingi kwamba mkulima atatumia nguvukazi yake kwa faida ya mabwanyenye kwenye vyama vya ushirika na Serikali. Pia kwa faida ya wafanyabiashara na taasisi za fedha.

Mkulima wa tumbaku anakopeswa pembejeo kwa bei kubwa ambayo sio halali. Anapouza anakatwa makato mengi hata kwa mambo ambayo hajatumia.

Mfumo mzima ni wa kinyonyaji. Hakuna mtu anayemsemea mkulima. Bado vyama vya ushirika vinashikwa na wanasiasa ambao nao wanafaidika na mfumo huo wa kinyonyaji. Nguvu wa mkulima ni ndogo na mkulima anakuwa kwenye mnyororo wa umasikini wa kutupwa. 

Mwalimu Nyerere alitahadharisha jambo hili katika Azimio la Arusha. Tumelisahau jambo hili.

Tunapofanya kumbukizi za Mwalimu turejee Azimio na nafasi ya kilimo katika maendeleo ya nchi. Sio kilimo cha wakulima wakubwa kinachopigiwa debe hivi sasa, bali kilimo cha wananchi walio wengi na wanaoishi vijijini. Tusisahau jambo hili.

Credit to: http://www.mwananchi.co.tz/uchambuzi/Azimio-la-Arusha-lilikufa-na-kilimo-vijijini/-/1597604/2031514/-/lols78z/-/index.html

No comments:

Post a Comment

© 2012 Designed by My Blogger Tricks