Study in South Africa: (www.southafricauniversities.blogspot.com) or Uganda: (www.ugandauniversities.blogspot.com)

Pages

Friday, October 11, 2013

Jaji Willy Matunga: Nafurahi kuwa mwathirika wa virusi vya Azimio la Arusha

NA SALOME KITOMARY.

Moja ya mambo yanayolikwaza taifa letu ni kuporomoka kwa maadili ya viongozi ambao hawafuati misingi ya  maadili katika ofisi za umma.

Hali hiyo inayosababisha viongozi hao wafyonze rasilimali za serikali ambazo zingeweza kuwa na manufaa kwa watu wengi lakini sasa zinaishia kuwanufaisha watu wachache.

Hapo ndipo wengi wanapotamani kurejeshwa kwa Azimio la Arusha ili kusaidia kuwahoji viongozi watakaoonekana wamejinufaisha kupitia ofisi za umma, watu wenye utajiri usiokuwa na maelezo ya kutosha.

Ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka, kutapanya mali ya umma, mikataba mibovu kwenye sekta mbalimbali ikiwamo madini na kujilimbikizia mali kwa baadhi ya viongozi wa umma kumeamsha kilio kwa watanzania wengi.

Machungu yameonekana zaidi miaka ya hivi karibuni, kutokana na huduma muhimu za kijamii kama maji, barabara, afya na elimu, kufifia na kutokidhi mahitaji ya watanzania kwa mapana yao.

Katika tamasha la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, lililofanyika katika ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kila mchangia mada alionyesha umuhimu wa kurejesha Azimio la Arusha na kuyatumia yaliyomo kwa vitendo.

Tamasha hilo lilikwenda sambamba na uzinduzi wa kitabu cha Miongozo miwili; Kupaa na Kutunguliwa kwa Azimio la Arusha, kilichoandikwa na wasomi watatu, Mwewnyekiti wa Kigoda cha Mwalimu,  Profesa Issa Shivji, Bashiru Ally na Saida Yahya Othman.

Jaji Mkuu wa Kenya, Dk. Willy Mutunga, katika siku ya tatu ya tamasha hilo alikuwa mgeni rasmi, mada kuu ikiwa ni Dira ya Maendeleo; Azimio la Arusha na Dira ya 2015.

Aliwasilisha tafakuri yake ‘Virusi’ vya Azimio bado vinaniandama, na kueleza jinsi anavyolitumia Azimio hilo nchini mwake katika kuleta usawa, haki na kuondoa ubaguzi ambao umekithiri nchini mwake.

“Nilifika Tanzania miezi 15 baada ya Azimio la Arusha, nikiwa mwanafunzi UDSM tulifanya midahalo kuchambua mtazamo wa Kwame Nkrumah na Mwalimu Julius Nyerere, juu ya mustakabali wa nchi za Afrika, walitufanya tuamini binadamu wote ni sawa na hadi sasa naamini hivyo,” alisema Jaji Dk.Mutunga

Anasema nchi za Afrika hususan Tanzania wanatakiwa kulirejea Azimio na kutekeleza kwa vitendo msingi yake, ambayo inakataa sheria za kibwenyeye.

“Navutiwa sana na misingi ya Azimio, ndio msingi wa kupinga sheria za kibwenyenye ambazo zinaletwa na nchi za Magharibi,” anasema

Jaji Dk.Mutunga anasema kutokana na kuvutiwa na misingi hiyo alipigania kazi ya Jaji ili kuifanya itumike nchini mwake, na amefanikiwa kuingiza kwenye Katiba yao aliyopigania kwa miaka 40.

Anasema licha ya nchi yake kuwa na ubaguzi wa kikabila, kidini, amejitahidi kujifunza kutoka Tanzania, lakini inashangaza kwa sasa misingi hiyo haitumiki na Azimio kutumika na wengine.
Anasema hatachoka kupigania usawa wa haki za binadamu kwenye nchi yake na kuishauri Tanzania kutolipuuza azimio na kurejelea misingi yake.

Dk. Mutunga ambaye alishiriki mchakato wa uanzishaji wa kituo cha sheria haki za binadamu (LHRC), anasema azimio lilisisitiza Umoja wa Afrika na kigoda hicho ni utambulisho wa Afrika.

Anasema ili nchi za Afrika zipige hatua kimaendeleo zinahitaji viongozi waliokuwa na uthubutu na jeuri kama Nyerere, ambaye hakukubali kuburuzwa na mataifa makubwa.

Matatizo ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika yatatatuliwa na katiba Mpya na ni aibu kuzungumzia Shirikisho la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakati muungano wa kwanza Afrika unakufa.

Aidha, anasema Azimio liliitambua lugha ya Kiswahili na kutumika kwenye shughuli mbalimbali, lakini kwa sasa imetupiliwa mbali na kukaribisha lugha za kigeni.

Anasema lugha inajenga utu, udugu na umoja wa kitaifa na itawezesha nchi za Afrika Mashiriki kujenga shirikisho bora.

“Najisikia raha kuwa mwathirika wa virusi vya Azimio la Arusha, ni kweli vinaniandama na nchi za Kibeberu haziwezi kuniingilia, tukikubali kuwa na virusi hivi kamwe hatutatawaliwa na sheria za kibwanyenye,” anasema

Anasema ni vigumu kwa nchi za Afrika kuendelea bila kujitegemea, hivyo vijana wamuenzi Mwalimu Nyerere na wengine kwa kuambukizana vizusi vya Azimio kwa kufanyakazi kwa bidii na si kuziimba fikra zao kama kasuku.

Anasema ni wajibu wa kila mtanzania kusambaza virusi vya Azimio, ili kuweza kujikomboa vinginevyo matatizo yataendelea kuliandama taifa.

Mwandishi Mwandamizi, Jenerali Ulimwengu, aliongoza malumbano ya mada ya Dira ya Maendeleo; Azimio la Arusha na Dira 2025.

Anasema misingi ya Azimio bado ina nguvu hadi leo, kwani taifa lolote haliwezi kuendelea kwa kutegemea kilimo cha wakulima wadogo na hakuna kiwanda cha kutengeneza zana za kilimo.

“Katika Azimio kuna miiko ya uongozi, ilipoondolewa tukaruhusu mtu yoyote kuwa kiongozi kwa kujaza fomu, kuambatanisha na kitita cha fedha ndio unakuwa kiongozi,” anasema
Anasema ipo sekretarieti ya maadini ya viongozi wa umma, ambayo taarifa huwa siri na viongozi huanisha mali walizonazo na taarifa zake kuwa siri.

“Mtu anaeleza ana nyumba mbili, kumbe ana 20 na zote kazipata kwa rushwa…mwandishi akizipata taarifa hizo na kuandika anashtakiwa, miiko ya viongozi haipo kabisa,” anasema Ulimwengu.

Vijana wanapaswa kuongoza mapambano kuongeza uwajibikaji na kukataa kutumika kwa maslahi ya kiasisa vinginevyo wataongozwa kwa lengo la kujipatia madaraka ni lazima kurejea kwenye dira.

Anasema aliye na sifa za uongozi hawezi kutoa fedha ili kulaghai watu na hakuna nchi inayoweza kuendelea bila dola kujihusisha na uchumi wa nchi yake.

Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Gombale Mwiru, alikuwa mchangiaji wa kwanza, anasema tatizo si kulitupa Azimio la Arusha, kwani masuala ya siasa ya ujamaa na kujitegemea linataka watu wawe pamoja.

“Kwa sababu ya ulegevu kwenye dhamira, watu wameweka maslahi binafsi mbele usimamizi wa ibara ya 18 ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, hiki si kikao cha chama ningesema zaidi,” anasema Kingunge na kuongeza;

“Viongozi wa serikali wanatakiwa kujaza fomu za kueleza mali zao, wengi hawajazi, nani anasimamia na kufuatilia?, wengine kila mwaka tunaandika mali zetu lakini tunanyooshewa vidole na wananchi kuwa ni wezi…zingekuwa wazi ingesaidia,” alilalama

Anasema utekelezaji wa Azimio unahitaji msimamo na bidii binafsi  kujenga umoja wa kitaifa na Tanzania ingepata viongozi kama Jaji Dk. Mutunga, ingefika mbali.

Aidha, alieleza kwa uchache kilichotokea wakati wa uanzishwaji wa miiko ya viongozi, anasema waliona ili kuwa na serikali imara lazima viongozi waachane na matumizi ya madaraka yao kujinufaisha, kuwa na mishahara miwili na nyumba ya kupanga.

Anasema mengi yaliwekwa kwa mazingira ya wakati ule na yanaweza kurekebishwa kuendena na mazingira ya sasa na kila lililopo ndani ya Azimio limepitwa na wakati.

“Tulichokosea wakati ule ni kuchukua miiko ya uongozi na kuifanya ndio shatri la kuwa mwanachama wa CCM, tulifanya ushabiki, jambo likiwa kwa ushabiki unazaa unafiki,” anasema
“Mwalimu Nyerere baada ya kung’atuka madarakani, alipewa zawadi nyingi na wananchi na aliniita mimi na na Rais Al Hassan Mwinyi, na kueleza kyuwa kutokana na zawadi nyingi alizopewa hana sifa tena za kuwa mwanachama kwa kuwa ana mali nyingi kinyume na katiba ya CCM kwa wakati huo,” anasema.

Anasema tatizo lilianza kuonekana na kuwalazimu kupitia upya na aliandika taarifa kuonyesha kuchanganya miiko ya viongozi kuwa ndio masharti ya kuwa mwanachama kumeleta utata na kuwanyima wengine haki ya kuwa wanachama mfano wenye nyumba za kupangisha.

“Mwaka 1967 mimi na wenzangu tulitumwa na Nyerere kuzungumza na mabalozi wa nyumba kumikumi Dar es Salaam, wengi walitutuma tumweleza mwalimu watawezaje kuishi bila kupangisha na mjini hakuna mashamba? Tulibaini tumekosea,” anasema

Naye, Profesa Samuel Wagwe, anasema kuna haja ya misingi ya Azimio kuingizwa kwenye mitaala ya kufundishia ili wanafunzi wajifunze tangu shule za msingi hadi vyuo vikuu.

Anasema dira ya maendeleo haikuwa ya kisiasa lakini iliweza kuzungumza na viongozi wa vyama vyote isipokuwa kimoja.

“Huwezi kutaja misingi ya Azimio na kuacha Dira, kuna mambo matatu ambayo ni utawala bora, kuinua hali za maisha na kujenga uchumi imara wenye kuhimili ushindani,” anasema 

Profesa Wangwe anasema njia pakee ya kuimarisha uchumi ni kuwekeza kwenye rasilimali watu.
Anasema utekelezaji wa dira hakufanyika hadi mwaka 2010 ndio serikali ikuanza utekelezaji kwa miaka mitano, jambo ambalo linaonyesha serikali iliendeshwa bila dira.

Baadhi ya wanafunzi wa UDSM, John Joel, Jaffari Habibu na Sadra Salehe, wanasema tofauti ya kipato kati ya aliyenacho na asiyenacho inazidi kukua na kupoteza malengo ya Azimio.

Wanasema ni lazima kuirejelea misingi ya Azimio la Arusha ambayo ina miiko kwa viongozi na kuondoa matumizi mabaya ya madaraka na kujilimbikizia mali huku watanzania wengi wakiogelea kwenye umaskini.

Naye, Balozi Getrude Mongelala, anasema miaka ya nyuma kila jambo ikiwemo masomo yalihusisha Azimio, kiasi cha kuwezesha kusambaa kwa kila mtazania.

“Kwa sasa kila mmoja amevaa kondomu kuzuia virusi vya Azimio, toeni kondomu tuende kwenye mapambano, matatizo ya jamii yanatokana na usawa na utu kutoweka,” anasema

Mhadhiri Mstaafu wa UDSM, Profesa Karsten Legere, anasema Azimio lina mengi mazuri kuliko yaliyopitwa na wakati ikiwemo matumzi ya lugha ya Kiswahili katika kuandika majengo mbalimbali, ambalo limeachwa na sasa lugha ya kiingereza kutawala kila mahali.

Mwenyekiti wa Chama cha majaji wastaafu, Jaji Thomas Mihayo, anasema nchi ilipofika inahitaji mapambano ili kufikia maendeleo kwa viashiria vilivyopo.

Anavitaja ni kama maandamano ya amani na halali, ambayo polisi hutumia nguvu na kusababisha umwagaji damu.

Credit to: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

© 2012 Designed by My Blogger Tricks