Study in South Africa: (www.southafricauniversities.blogspot.com) or Uganda: (www.ugandauniversities.blogspot.com)

Pages

Sunday, October 13, 2013

Azimio la Arusha liliishia Chumbe, leo hali ikoje?

Na Juma Mohammed, China.
   
MALUMBANO yanayoendelea kuhusu Katiba mpya hayaoneshi kuwa tunaweza kufikia na kupata Katiba bora inayotokana na matakwa ya wananchi wenyewe. Nasema hivi kwa sababu hata Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, tayari ameonesha wasiwasi na kutoa angalizo kutochezewa kwa maoni ya wananchi waliyotoa kuhusu aina ya Katiba wanayoitaka.

Haieleweki ni kwa mazingira gani hadi tumefikia hatua iliyotuingiza kwenye malumbano yasiyo na tija kwa umma, lakini kwa upande wa pili malumbano hayo ni dalili ya watu kutoridhika jinsi mambo yanavyofanyika au yanavyoendelea.

Sina sababu ya kurejea hali iliyosababisha kupitishwa kwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba, 2013 bungeni, wengi tunafahamu kilichotokea.

Jambo moja linalonishangaza ni kwamba Muungano huu ni wa nchi mbili; Zanzibar na Tanganyika, zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inakuwaje Zanzibar ionekane kama mgeni mwalikwa?

Tumesikia mambo yalivyokuwa wakati wa mchakato wa kutafuta maoni kuhusu mswada huo ulivyolalamikiwa Wazanzibari!

Zanzibar ikiwa mshirika sawa katika Muungano, wananchi wake walikuwa na haki ya kutoa mawazo yao katika suala hilo kwani wao ndio wenye maamuzi ya mwisho kuhusu nchi yao na si vyenginevyo.

Yetu sie macho, lakini hatuna budi kueleza kwamba chini ya mfumo uliopo wa Muungano, itakuwa vigumu sana kuiona Zanzibar ikijitanua katika uwanja wa kimataifa.

Inafahamika na kila mtu kwamba kazi ya kukuza uchumi kwa Zanzibar chini ya Muungano wa sasa ni ngumu kama ilivyo vigumu kukuna nazi na mbuzi isiyo na meno!

Katika miaka 49 ya Mapinduzi, maendeleo ya Zanzibar kiuchumi yamekuwa ni ya kusuasua huku mwendokasi wa uchumi ukiwa sawa na wa chura, wa kurukaruka hapa na pale; sijui tutafika lini kwenye kilele cha maendeleo endelevu na kutimiza malengo ya MDG.

Tatizo la ajira kwa vijana, uhaba wa vyuo vikuu ambavyo vingeweza kuandaa vijana katika soko la ajira la ndani na lile la kimataifa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina miliki Chuo Kikuu kimoja tu katika miongo minne ya kujitawala; Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Hospitali ya Mnazi Mmoja haijafikia vigezo vya kuitwa Hospitali ya Rufaa, hadi sasa hadhi yake ni sawa na Hospitali Kuu; hakuna Hospitali ya Mkoa au teule kama Tumbi, Kibaha; Zanzibar kuna hospitali za ngazi ya vijiji kama Kivunge mkoa wa Kaskazini Unguja na Makunduchi, Kusini Unguja.

Pemba kuna hospitali ambazo sina hakika kama ni za mkoa au wilaya; Abdallah Mzee ipo Kusini Pemba na Wete ya Kaskazini Pemba. 

Serikali yoyote duniani inawajibu wa kuwapa wananchi wake huduma muhimu kama afya, elimu, makaazi, usafiri na pia kuwasaidia kupata ajira hasa vijana. SMZ ina mzigo mzito katika kufanikisha haya chini ya muundo uliopo wa Muungano.

Tunaweza kukumbuka kwamba nchi zilizokuwa zikitawaliwa zilianzisha mapambano, awamu kwa awamu, ili kujikomboa kuondokana na madhila ya ukoloni ziwe huru kujiamulia mambo yake zitakavyo kulingana na matakwa ya wananchi wake.

Wazanzibari, kama ilivyokuwa kwa wananchi wa nchi nyingine, hususan za dunia ya tatu, walipigania uhuru. Hatimaye uhuru ukapatikana Desemba 1963 pale bendera ya Kiingereza iliposhushwa na kupandishwa ya Zanzibar huru. 

Hata hivyo, wananchi wengi wa Zanzibar hususan wanachama wa Afro Shiraz Party hawakupenda kitendo cha mkoloni mmoja kuondoka kisha kumpatia uhuru huo mkoloni mwingine, Sultan.

Tunaelewa kwamba Sultan hakuwa miongoni mwa wakoloni waliokutana Berlin, Ujerumani, mwaka 1884-1885 katika mkutano maarufu wa kinyang'anyiro cha mgawanyo wa Bara la Afrika ambapo Wazungu waligawana ardhi ya Afrika kama yao, tena kwenye meza wakichora ramani wanayoitaka. Wazanzibari hawakuridhia hali hiyo. 

Kimsingi ASP na Wazanzibari kwa ujumla wao waliamini kuwa kuendelea kwa Sultan kubaki kama mkuu wa nchi ilikuwa ni kuendeleza ukoloni kwa mlango wa nyuma na wakatafsiri kuwa hicho ni 'kiwingu' cha aina fulani juu ya uhuru walioupata mwaka 1963. 

Hivyo, ASP kikawaongoza wazalendo wa kike kwa kiume usiku wa kuamkia Januari 12, 1964, wakaingia bomani na kufanikiwa kukiondosha kiwingu hicho na Zanzibar huru ikazaliwa na bendera mpya ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ikaanza kupepea kila kona.

Kila pembe salamu zilikuwa “uhuru na bwana Abeid” wengi walifurahia kuona Zanzibar imekuwa Jamhuri na kutangazwa jina jipya la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Baadhi yenu mnaweza kuuliza, kwanini wananchi wa Zanzibar waliamua kufanya Mapinduzi? Jawabu ni jepesi sana kwani walitamani na waliamua kuwa huru, kuwa na uhuru wa kujiamulia mambo wenyewe bila kuingiliwa na yeyote asiye Mzanzibari au asiyetetea maslahi ya Zanzibar. 

Waasisi wale wa Mapinduzi, jemedari Abeid Amani Karume, Ramadhan Haji Faki, Sheikh Thabit Kombo Jecha, Brigedia Yussuf Himid, Kanali Seif Bakar, Khamis Darwesh na wengineo, waliamua na walipanga kuiendesha nchi yao katika namna wanayoona inawafaa.

Na zaidi kuona kwamba hawaingili uhuru wa nchi nyingine kama ambavyo wao wasivyopenda wasiingiliwe na mwengine katika kuendesha mambo ya nchi yao kwa manufaa ya watu wake.

Hiyo ndio sababu ya kipekee wananchi chini ya ASP kuamua kuufukuza utawala wa kikoloni wa Sultan na aila yake.

Miaka 49 sasa tangu Mapinduzi matukufu kuelekea miaka 50 hapo mwakani, suala la kuuliza dhamira ya Mapinduzi yale imefikiwa na yale yalokusudia kuipa Zanzibar uhuru wa kweli na kile 'kiwingu' juu ya uhuru wao kimeondoka au kimezidi kutanda katika anga la nchi yao na hivyo kufanya kiza kinene kutanda?

Je, Zanzibar kama nchi inaweza kujiunga na mashirika makubwa kama OIC, FAO, FIFA na mengineyo? Ni dhahiri kuwa kwa muundo wa sasa wa Muungano, Zanzibar haina ubavu wa kuingia mikataba ya kimataifa bila kuomba kibali cha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwaka jana Waziri (mwandamizi) wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini alisema katika mkutano mmoja kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisaini mkataba wa Zanzibar licha ya kutohusika nao wakati Waziri Mwinyihaji ndiye aliyepaswa kufanya hivyo!

Sipati picha kama Rais wa Kwanza wa Zanzibar huru na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu Karume angekuwa hai na mambo yanavyokwenda katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Sina hakika kama angesemaje pale Dk. Salmin Amour Juma alipotakiwa kuiondoa Zanzibar uanachama wa OIC.

Pia sipati picha kama Karume angekuwepo na kauli hizi za "msitikise kiberiti" au Zanzibar kutokuwa hata mwanachama wa FIFA wakati suala la michezo na burudani si la Muungano. 

Zanzibar ina chama chake cha soka na Bara inacho cha kwake; vipi TFF inapata uhalali wa kuwa memba wa FIFA huku ZFA ikikosa?

Waliokula chumvi nyingi bado wanakumbuka namna Wazanzibari wengi walipoonesha hofu ya nchi yao kutaka kumezwa kwa visingizio vya 'Sera za Chama kushika hatamu' na Azimio la Arusha, Rais wa Zanzibar kwa wakati huo, Abeid Karume, aliwaondoa hofu Wazanzibari kwamba wasiwe na wasiwasi kwani Azimio la Arusha lingeishia Chumbe.

Miaka 46 baada ya Azimio la Arusha na kauli ya Karume na namna tunapoitazama hali ya mambo katika mfumo wa muundo wa Muungano wetu ni kweli mambo ya kuingilia uhuru wa Wazanzibari yameishia Kisiwa cha Chumbe kama alivyoahidi Marehemu Karume?

Ni kitendawili ambacho kinaweza kuanguliwa katika mfumo mpya unaopendekezwa na wengi wa Serikali tatu ambao utaifufua Tanganyika ili Zanzibar iweze kumuona mshirika mwenzake badala ya kivuli.

RAI: http://www.rai.co.tz/index.php?option=com_content&view=article&id=513:azimio-la-arusha-liliishia-chumbe-leo-hali-ikoje&catid=5:siasa&Itemid=35

No comments:

Post a Comment

© 2012 Designed by My Blogger Tricks