Study in South Africa: (www.southafricauniversities.blogspot.com) or Uganda: (www.ugandauniversities.blogspot.com)

Pages

Friday, October 11, 2013

Tufuate Azimio la Zanzibar au Azimio la Arusha?

Na Deusdedit Jovin.

TANGU kuzaliwa kwa taifa letu, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alisanifu “KANUNI YA UTANZANIA”, kanuni ambayo ilifafanuliwa zaidi kupitia Azimio la Arusha mwaka 1967 na pia kupitia matamko mengine yaliyofuata baada ya hapo.

Kwa mujibu wa historia, “Azimio la Arusha” liliasisiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU iliyokutana “Arusha Community Centre” kuanzia Januari 26, 1967 hadi Januari 29, 1967. Baadaye lilithibitishwa na Mkutano Mkuu wa TANU mwezi Machi 1967 (Nyerere: Ujamaa, 1968, uk. 13 & 33).

Uamuzi huu ulikuwa ni mwendelezo wa azma ya chama cha TANU ya kujenga Taifa la Kijamaa kama ulivyokwishafanyika tangu mwaka 1962 (Nyerere: Ujamaa, 1968, uk. vii).  Azimio hili linahusu “Ujamaa”, yaani mfumo wa kiuchumi, kijamii na kisiasa unaowezesha umma kumiliki njia kuu za kuzalisha mali na mgawanyo wa haki wa mapato ulioasisiwa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Azimio hili limefafanuliwa vizuri katika kitabu kiitwacho “Ujamaa” kilichochapishwa jijini Dar es Salaam, kupitia kampuni ya uchapaji iitwayo “Oxford University Press” mwaka 1968. Katika kitabu hiki, “Azimio la Arusha” limejadiliwa katika sura ya pili, kuanzia ukurasa wa 13 hadi 35.

Kwa kuwa sasa tunaelekea katika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge, msimu ambao unahitaji sana kuziongoza akili za wapiga kura kwa kutumia kanuni zisizobadilikabadilika kama kinyonga, na kwa kuwa, ninaamini kwamba kanuni za aina hii zinapatikana katika Azimio la Arusha, leo nimeamua kuzifanyia muhtasari kanuni hizi kwa faida ya wasomaji na wapiga kura kwa ujumla.

DIRA ASILIA YA TAIFA LA TANZANIA

Kitu cha kwanza tunachokiona katika Azimio la Arusha ni Dira Asilia ya Taifa la Tanzania. Kimsingi, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba: “Siku moja tutaishi katika taifa lenye serikali ambayo, kwa kuzingatia kanuni ya ruzuku, inafanya kazi usiku na mchana ili kukuza na kuhami usawa wa binadamu kwa kutekeleza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea katika namna ambayo inakuza maslahi ya pamoja na kuhami maslahi ya kila mtu binafsi.”

Hii ndio  DIRA YA TAIFA la Tanzania tangu mwanzo, dira ambayo inafafanuliwa zaidi katika mchoro hapa chini.

FALSAFA YA TAIFA LA TANZANIA 

Hata hivyo, mtu hawezi kuilewa vema dira asilia ya Tanzania, endapo haelewi msingi wake; yaani falsafa ya kijamii inayozingatiwa na Azimio la Arusha. Yaani, dira ya taifa la Tanzania imejengeka katika msingi imara wa kanuni zilizotajwa katika Azimio la Arusha.

Na hapa ni mapendekezo yangu kwamba zipo kanuni kumi na mbili, kanuni ambazo zinatajwa kwa kifupi hapa chini, na kanuni ambazo kwa ujumla wake ndio nazirejea kama “falsafa ya kijamii” (social philosophy) inayozingatiwa na Watanzania tangu mwanzo.  Kanuni hizi ni kama ifuatavyo:

Mosi, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba, “Binadamu wote, kama sehemu ya ufalme wa wanyama ambao wanatofautishwa na hazina yao ya uwezo wa kufanya mang’amuzi, kufikiri na kufanya maamuzi huru mintarafu matendo, malengo na mazingira ya utekelezaji wa matendo hayo, huzaliwa wakiwa na hadhi sawa.” Hii ni KANUNI YA USAWA WA UBINADAMU (the principle of human equality).

Pili, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba: “Kila tendo la binadamu linawezekana pale tu ambapo kuna uhuru wa kuchagua na kutenda, ambapo uwezekano wa kutenda unawekewa vikwazo na mazingira ya kijamii, kimaumbile na kimiujiza, na ambapo uwezekano huu unapungua kadiri ukubwa wa vikwazo unavyoongezeka.” Hii ni KANUNI YA UHURU WA MWANADAMU NA MIPAKA YAKE (the principle of human freedom and necessity).

Tatu, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba, “Binadamu wote wanazo haki zisizopokonyeka, zisizosiginika, na zisizofungwa na mipaka ya kitabaka, ambapo haki hizo ni pamoja na haki za kiuchumi, kijamii, kisiasa, kielimu, kijinsia, kuishi, kiafya, kujifaragua, na haki-mtambuka”. Hii ni KANUNI YA HAKI ZA BINADAMU (the principle of human rights)

Nne, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba: “Binadamu wote wanaweza na wanapaswa kutumia akili yao kujua kilicho chema kwao, kwa maana ya malengo, matendo na mazingira ya utekelezaji wa matendo haya, kama ambavyo wanaweza na wanapaswa kujiongoza wenyewe katika kufukuzia malengo mema kwa kufanya matendo safi, kuyaepuka matendo machafu, kuyapuuzia malengo maboovu, na kuyakimbia mazingira mabaya”. Hii ni KANUNI YA UADILIFU WA MATENDO YA BINADAMU (the principle of moral human acts)

Tano, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba:“Wanadamu wanapobaini ulazima wa kufanya kazi ambayo ni muhimu kwa ustawi wa kila mmoja wao, lakini kazi ambayo haiwezi kufanywa na yeyote kati yao, basi, huwa wanaunda jumuiya inayowajibika kwao, jumuiya  ambayo huwa wanaipatia kasma ya madaraka ya kufanya kazi hiyo, ambapo jumuiya hii huwa ni nyenzo ya kukuza maslahi ya pamoja, kwa maana ya jumla ya mafao  shirikishi yanayomwezesha kila mmoja wao kujitimizia maslahi yake binafsi.” Hii ni KANUNI YA UJAMAA (The principle of Socialism).

Sita, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba: “Wanadamu wasipobaini ulazima wa kufanya kazi fulani, ambayo ni muhimu kwa ustawi wa kila mmoja wao, na kazi ambayo haiwezi kufanywa na yeyote kati yao, basi, hawatahangaika kuunda jumuiya yoyote ambayo ingewajibika kwao, jumuiya  ambayo wangeipatia kasma ya madaraka ya kufanya kazi hiyo, hata kama jumuiya hii ingekuwa ni nyenzo ya kukuza maslahi ya pamoja.” Hii ni KANUNI YA KUJITEGEMEA (the principle of self-reliance)

Saba, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba: “Wakati wowote inapokuwepo jumuiya kubwa ambayo ndani mwake kuna jumuiya ndogo ndogo, basi, endapo jumuiya ndogo zinaweza kutimiza majukumu yake baada ya kuongezewa nguvu na jumuiya kubwa, ambapo nyongeza hiyo lazima iombwe na jumuiya ndogo, litakuwa ni jukumu la jumuiya kubwa kujizuia kuyatekeleza majukumu yanayoweza kutekelezwa vizuri zaidi na jumuiya ndogo.” Hii ni KANUNI YA RUZUKU (the principle of subsidiarity).

Nane, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba: “Kwa kuwa misingi muhimu ya maendeleo ya kiuchumi ni rasilimali watu, rasilimali asilia, na rasilimali zilizobuniwa na watu, ambapo rasilimali watu inajumuisha raia wenye ujuzi, afya njema na elimu bora, basi, ni lazima kutimiza mahitaji muhimu kama vile chakula, mavazi, malazi, huduma za elimu na afya, kama hatua ya kwanza katika safari ndefu ya kuzuia unyonyaji, kukuza uchumi, na kupunguza umasikini.” Hii ni KANUNI YA KUKUZA UCHUMI NA KUPUNGUZA UMASiKINI (the principle of economic growth and poverty reduction).

Tisa, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba: “Uendeshaji wa jumuiya za wanadamu kwa kufuata utawala wa sheria ndiyo ndiyo njia pekee ambayo kwayo ukweli, haki na wajibu vyaweza kukuzwa na njia pekee ambayo kwayo uwezekano wa binadamu kuteleza na hivyo akafanya ufisadi na kuhujumu haki vyaweza kuzuiwa.” Hii ni KANUNI YA UTAWALA WA SHERIA (the principle of the rule of law).

Kumi, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba: “Serikali ya nchi huundwa na wananchi ili ikakuze na kuhami ndoa iliyopo kati ya wananchi hao na maliasili zilizo nchini mwao ambapo serikali inatarajiwa kusanifu na kutekeleza sera na programu ambazo zitakuza maslahi ya pamoja, na ambapo serikali hii hupokea kasma ya madaraka kutoka kwa wananchi na kwa ridhaa yao kupitia sanduku la kura.” Hii ni KANUNI YA MAJUKUMU YA DOLA (the principle of state respinsibilities).

Kumi na moja, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba: “Kwa kuwa serikali ya nchi inawajibika kwa wananchi, basi, endapo serikali hii itahujumu maslahi ya pamoja, itakuwa ni haki ya wananchi kuyapinga maamuzi ya serikali au kuivunja serikali hiyo na kusimika serikali mpya, serikali ambayo itawajibika kuzingatia masharti yote, kama ambavyo yatawekwa na wananchi kwa ajili ya kukuza na kuhami maslahi yao ya pamoja.” Hii ni KANUNI YA UWAJIBIKAJI WA DOLA (the principle of state accountability)

Na kumi na mbili, Azimio la Arusha linatufundisha kuamini kwamba: “Katika nchi ambayo inajumuisha utitiri wa madhehebu ya dini, maslahi ya pamoja katika mipaka ya madhehebu, yanaweza kukuzwa endapo dini sio kigezo cha mtu kuingizwa katika ofisi ya umma, na endapo bunge halitatunga sheria inayoruhusu serikali kuanzisha na kuendesha shughuli za kidini au kuzuia uhuru wa kuabudu katika mipaka ya madhehebu.” Hii ni kanuni ya kutenganisha dini na siasa (the principle of religion-politics separation).

MAPENDEKEZO KWA WAPIGA KURA 2010

Hivyo basi, kwa kuwa “tumeonewa kiasi cha kutosha” na serikali ya CCM, tumenyonywa kiasi cha kutosha” na serikali ya CCM, “tumepuuzwa kiasi cha kutosha” na serikali ya CCM, na kwa kuwa “unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe, na kupuuzwa”; ni wazi kwamba “sasa tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena” wala kupuuzwa tena! 

Na njia pekee ya kufanikisha jambo hili ni kumuunga mkono mgombea yeyote atakayekuonyesha kwa dhati kabisa kwamba analielewa na kulikubali Azimio la Arusha kwa moyo wake wote. Lakini lazima niseme wazi kwamba, kwa kuzingatia Mwelekeo wa sera za CCM kati ya mwaka 2010 na mwaka 2020, CCM na wagombea wake nina shaka kuwa ni miongoni mwa hao!

Credit to: http://www.raiamwema.co.tz/tufuate-azimio-la-zanzibar-au-azimio-la-arusha

No comments:

Post a Comment

© 2012 Designed by My Blogger Tricks