Study in South Africa: (www.southafricauniversities.blogspot.com) or Uganda: (www.ugandauniversities.blogspot.com)

Pages

Friday, October 11, 2013

Jaji Joseph Sinde Warioba ataka Azimio la Arusha

Na Halima Mlacha.

ALIYEKUWA Waziri Mkuu Jaji Joseph Warioba, amesema anatamani Azimio la Arusha lirudi kwa kile alichoeleza kuwa, kwa sasa kuna mmomonyoko wa maadili kwani viongozi wengi wamekuwa wakithamini zaidi mali kuliko maslahi ya wananchi.

Amesema wakati sasa umefika kwa wananchi kutotegemea sheria kuwa itajenga msingi wa maadili kwa viongozi, bali matendo yao ndio yatajenga maadili hali ambayo inapelekea haja ya kufikiria kuwa na Azimio la Arusha la pili ili kulinda maadili hayo.

Akifungua mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) wa Vyama vya Siasi juu ya Maadili ya Viongozi jana Dar es Salaam, Warioba alisema iwapo Azimio hilo la pili litarudi hali ya sasa ya maadili ya viongozi itabadilika na matatizo mengi hasa ya ufisadi yatakwisha.

“Suala la maadili ya viongozi historia yake inaanzia zamani ambako, viongozi walikuwa wakijali zaidi maslahi ya wananchi kwa kufuata misingi ya Azimio la Arusha, labda kwa sasa umefika wakati wa Arusha nyingine ambako viongozi kama sisi tutakuwa na ujasiri wa Arusha ya 1967,” alisema Warioba.

Alisema bila vitendo vinavyoambatana na maadili sheria ni bure kwani uongozi huambatana na kujitolea na kujali zaidi, ndio maana kipindi cha Azimio la Arusha mwaka 1967, maadili ya viongozi yalikuwa ya juu tofauti na sasa ambako kumetawaliwa na matabaka.

Alisema viongozi wa kipindi hicho cha zamani walikuwa wakifuata maadili yao pamoja na miiko iliyopo ndani ya azimio hilo ambayo ni ili uwe kiongozi ni lazima uwe mkulima au mfanyakazi, usiwe na hisa katika kampuni yoyote, usiwe mkurugenzi wa bodi au kampuni binafsi, usiwe na mishahara miwili na usiwe na nyumba ya kupangisha.

“Ingawa mambo haya yaliwekwa kwenye kanuni za kazi, watu waliafuata azimio bila ya kujisumbua sana na kanuni zilizoandikwa, wala haikutungwa sheria maalum kwa ajili ya Azimio, wananchi waliyajua masharti ya uongozi na walishiriki kuhakikisha viongozi wanayatekeleza,” alisema.

Alisema haikuwa pia rahisi kwa kiongozi kuvunja miiko hiyo.”Nampongeza sana Aliyekuwa Waziri Mkuu Rashid Kawawa kwani pamoja na kuwa kiongozi wa juu wakati ule pengine baada ya Malkia Elizabeth, maisha yake mpaka sasa ni ya kawaida hayafanani na nafasi aliyonayo,”

Jaji Warioba alisema Azimio la Arusha lilikuwa linazingatia kuwa fedha si msingi wa maendeleo bali ni matokeo, hali ambayo kwa sasa ni kinyume kwani sasa fedha imekuwa ndio msingi wa uongozi kwani ndio unaoonekana kuwa njia ya kujitajirisha.

Alisema kutokana na hali hiyo sasa kumekuwa na matabaka ambapo mkulima na mfanyakazi sasa hawana tena nafasi ya kuwa viongozi bali wenye mali au wenye uhusiano wa karibu na wenye mali na wakitaka kuondolewa inaleta uadui hadi kwenye vyama vya siasa.

Alisema sasa anaamini kuwa kuna makosa yalifanyika katika kufuta baadhi ya vitu vya azimio hilo hali ambayo imesababisha watanzania wengi kupoteza ujasiri wa kujitegemea na kubaki na dhana kuwa kila kitu kinawezekana kwa kutegemea ufadhili.

“Katika kipindi nilichokuwa kiongozi kila kitu nilikuwa nafanya kwa kutegemea mshahara wangu tu, tofauti na sasa viongozi wengi mshahara ni sehemu ndogo tu ya mapato yao, kwani wana marupurupu mengi kama posho ambayo yanazidi mshahara husika,” alisema.

Alisema kwa sasa hali ni ngumu, kwani matabaka yanaonekana wazi viongozi wengi wanaonekana kujali maslahi yao zaidi. “Sasa hivi kima cha chini ni 100,000 wakati mshahara wa juu kabisa ni mamilioni, zamani viongozi walikuwa tayari kutoa uamuzi mgumu kupunguza mishahara yao, tofauti na sasa,”

Alisema ili matatizo hayo yaondoke na uadilifu wa uongozi urejee kama zamani, viongozi hawana budi kufuata maadili kwa vitendo ikiwa ni pamoja na Azimio la Arusha kufikiwa kurejea tena ili liwaongoze.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, alisema semina hiyo imelenga kuwaunganisha viongozi wote wa siasa bila kujali itikadi zao ili kuzungumzia namna ya kutetea nafasi zao kwa kuzingatia maadili ya uongozi.

Alimsifu Jaji Warioba kuwa ni kiongozi makini ambaye amekuwa mstari wa mbele kusimamia maadili tangu kipindi cha awamu ya kwanza na yupo wazi kukosoa kwa vile anavyoaamini yeye hali ambayo inapaswa kuigwa na viongozi nchini.

Credit to: http://www.nifahamishe.com/NewsDetails.aspx?NewsID=350898&&Cat=1

No comments:

Post a Comment

© 2012 Designed by My Blogger Tricks