Na M. M. Mwanakijiji.
NINAZO habari nzuri na habari mbaya. Habari nzuri ni kuwa hatimaye sasa tunajua kuwa waliozika Azimio la Arusha wamegundua kwamba walifanya makosa. Habari mbaya ni kuwa chama kilichosimamia maziko ya Azimio hilo hakiwezi kamwe kulirudisha.
Ni kwa sababu Azimio bado halijafa. Waliolizika wamesahau kulivalisha sanda, na wamelifukia bila kuliswalia! Hata jaribio la miaka 20 la kutaka wananchi walisahau limeshindwa. Ndugu zangu, Azimio la Arusha bado liko hai, ondoeni msiba na anueni matanga!
Ni kwa sababu, waliolizika azimio wamesahau jambo moja muhimu sana, kwamba mawazo au fikra haviwezi kufa. Wala falsafa haiwezi kufutwa kwenye kikao hata kama kikao hicho kimefanyika mbinguni. Fikra bora hupita kizazi kimoja kwenda kingine na kama pumzi ya uhai kupitishwa toka kwa wazazi kwenda kwa mwana katika utaratibu ambao ni mbinguni tu wanaweza kuubuni.
Kwa vijana wengi na hata wazee ambao wamelisikia Azimio na kulisoma, wameshindwa kuelewa utajiri uliofichika ndani ya Azimio hili. Leo hii tukilitaja Azimio hili wapo ambao kijasho kinawatoka.
Ukiwauliza watu wengi, Azimio lilihusu nini, watakimbilia kusema “utaifishaji.”Lilifanya nini wengi watakimbilia kusema, “lilisababisha operesheni vijiji vya ujamaa.” Wengine watakwambia haraka kuwa “hilo halina nafasi yoyote katika Tanzania ya leo.”
Lakini ukiwauliza kama wamebahatika kulisoma, hakika utashangaa.
Rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi ametoa maelezo mazuri kuelezea kwa nini Azimio la Arusha limekuja na kile kilichotokea Zanzibar ambacho baadaye kimekuja kujulikana kama Azimio la Zanzibar.
Amesema, “…Tanganyika ilipopata uhuru na tukaanza kujitawala, ishara potofu zilianza kuchomoza. Baadhi ya viongozi walianza kuutumia uongozi wao kama mradi wa kujineemesha. Kwa kutumia nyadhifa zao, walikopa fedha benki na kuanza kujijengea mashamba - si ya miti - bali ya majumba; si nyumba za kuishi tu bali majumba mengi ya kupangisha.
“Tabia hiyo ilizusha manung’uniko. Jamii ilianza kugawanyika makundi mawili; manaizi na makabwela. Kitendo hicho ndio chimbuko la kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Azimio lilikuja kutoa mwongozo wa maadili ya wanachama na viongozi wa TANU. Kwa hivyo, nia ya Azimio la Arusha, miongoni mwa mambo mengine, ilikuwa ni kuwazuia viongozi kutumia uongozi wao kujitajirisha. Hilo ndilo lililokuwa tatizo la hatari miongoni mwa matatizo ya wakati ule. Azimio lilikuja kuokoa jahazi – kukemea tabia potofu.”
Tunaona kuwa azimio lilikuja “kuokoa jahazi” na sababu ni kuwa kulikuwa na manung'uniko kati ya wananchi na viongozi waliokuwa wakitumia madaraka yao vibaya.
Je, hali ya leo siyo ile ile iliyokuwepo wakati Azimio linatangazwa? Si kweli kwamba hivi sasa, wananchi wana manung'uniko mengi kwa viongozi wao kuhusu mali zao na jinsi wanavyotumia nafasi za umma kujitajirisha?
Je, si kweli kwamba hata mtoto wa rais Mwinyi alijipatia kiwanja – kilichokuwa kimetaifishwa wakati wa Azimio la Arusha na kisha yeye kujenga jumba la kupangisha wakati ni kiongozi wa umma?
Azimio lilikuja na lengo kubwa zaidi. Ilikuwa ni ramani ya taifa ambayo tulitaka tuifuate. Ni mchoro wa jengo tunaloliita taifa. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alilieleza hili katika hotuba yake ya 5 Agosti 1967 aliyoitoa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara baada ya Azimio kutangazwa.
Alisema, “…Azimio la Arusha linaweka shabaha ya mendeleo. Tanzania haikuwa nchi ya Ujamaa ghafla siku ile ile ya tarehe tano Februari, au siku yoyote tokea hapo; wala kwa sababu hiyo tu Tanzania haijawa nchi yenye kujitegemea, au nchi iliyoendelea.”
Kwamba Azimio lisingeweza kufanya mambo hayo siku hiyo hiyo; wala isingewezekana, hata kama watu wangekuwa na ari, au nguvu kiasi gani, kutimiza shabaha hizo katika miezi michache tangu Azimio lipitishwe.
Mwalimu Nyerere alifika mbali zaidi. Alisema, “Mtu anayejidai kulitumia Azimio ili limpe haki ya kuwasakama watu wa rangi fulani, au anayelitafsiri Azimio kama linashambulia watu wa rangi fulani, anadhihirisha upumbavu wake, na pia anavyoyakataa mambo yaliyomo katika Azimio.”
Hivyo basi, Azimio hili lilikuwa ni zaidi ya uamuzi wa kutaifisha mali. Wengine walifikiri kuwa Azimio lilikuwa dhidi ya Wahindi na Wazungu.
Alipotangaza Azimio la Arusha Mwalimu alikuwa anatangaza ramani ya nchi kwa lengo la kuonyesha taifa gani tunataka kulijenga.
Hivyo basi, wale wanaotaka Azimio lirudi wajue kabisa kuwa wanachotaka ni kutaka kuangalia ramani yetu ikoje.
Wamarekani kwa mfano wanasonga mbele na kuendelea, lakini mara zote wanarudi na kuangalia ramani ya ujenzi wa taifa lao kama ilivyotangazwa katika Azimio lao la Uhuru 4Julai 1776 na kuandikwa vizuri kwa kina katika Katiba yao (na mabadiliko yake yote).
Huwezi kuwaambia kitu Wamarekani kuhusu uhuru wao kama taifa na kama mtu mmoja mmoja; huwezi kuwaeleza juu ya haki ya kujieleza na kutoa maoni yao; na huwezi kuwaambia kitu kuhusu uwezo na haki ya wananchi wao kuisimamia serikali yao.
Leo hii watu wanawahusudu Wamarekani na wanaihusudu Marekani, wanadhania nchi hiyo imeteremshwa iliyopambwa kama Yerusalemu kutoka mbinguni.
Marekani ni nchi iliyozaliwa kutokana na damu; imezaliwa kutokana na Azimio lao la Uhuru; azimio ambalo halikuwafurahisha watu wote. Zipo taarifa kwamba katika kujenga nchi hiyo, mamia ya watu wamepoteza maisha kulinda azimio hilo. Leo hii, Wamarekani wanakula katika kivuli ambacho wazazi wao walichumia.
Kumbe basi Azimio letu kama alivyosema rais Mwinyi na Nyerere, lilikuwa ni azimio la “shabaha” la nini tunataka kufanya katika nchi yetu. Kutoka na kuzikwa bila kuliswalia, taifa letu linaongozwa kwa kubahatisha.
Matatizo ambayo azimio liliona miaka 40 iliyopita, yapo mpaka sasa na mengine yamekua zaidi. Kwa sababu tuliacha kujenga taifa kwa misingi tuliyoitaka na tukakubali matakwa ya wachache waliosema azimio ni baya na linarudisha nyuma maendeleo.
Bali, Azimio la Arusha lilikuwa ni dira. Leo hii, kila kiongozi anakuja na mpango wake. Yupo aliyekuja na kauli mbiu ya ruksa, mwingine “uwazi na ukweli” na huyu wa sasa amekuja na “Kasi Mpya, Ari Mpya na Nguvu Mpya.”
Hakuna hata mmoja ambaye anaweza kutaja neno “Azimio la Arusha” hadharani; kukiri kuwa nchi ilikuwa na ramani na kwa hakika hasisitiza kulirudisha. Wala CCM hakiwezi kurudisha Azimio la Arusha. Hakiwezi kwa sababu, azimio linasimama kama hati ya mashtaka dhidi ya chama hicho.
Azimio lile linaogopwa na wanyonyaji mambo leo na kwa hakika, wanyonyaji hao siyo Wahindi wala Wazungu! Ni CCM. Iwapo ikikumbatia azimio la Arusha, kina Kingunge watakula wapi?
Wanyonyaji wanaotajwa kwenye Azimio la Arusha ndio tumewabadilisha jina na kuwaita mafisadi. Hii ni kwa sababu watu hawataki kuitwa tena wanyonyaji. Azimio la Arusha halikumtisha mtu aliyetaka kutengeneza maisha yake kwa uhalali; halikuwa tishio kwa vijana na wazee ambao walitaka nafasi sawa ya kufanikiwa katika nchi yao. Azimio lilitoa nafasi kwa wananchi wote bila kujali rangi, kabila, dini, au hali ya maisha kufanikiwa katika maisha yao.
Hivyo, wale wanaotaka Azimio lirudi ni muhimu watambue kuwa kile wanachokitaka ni kikubwa kuliko maadili ya uongozi au miiko ya uongozi iliyomo kwenye azimio hilo. Wanaotaka Azimio lirudi wajue wanalilia ramani ya taifa letu; wanataka mchoro wa ujenzi wa nchi yetu ambao CCM wameukana.
Mwaka huu wa uamuzi, Watanzania watatakiwa kujiuliza kama wanataka kuendelea kujaribu kujenga nchi bila kufuata dira yoyote inayoeleweka au kufanya kila ambacho nchi nyingine zimefanya.
Azimio la Arusha likirudishwa Tanzania, yawezekana ukawa ni mwanzo wa ukombozi mpya wa taifa letu na kurudi pale tulipopotea. Azimio halikufa kama tunavyotakiwa tuamini; halikuzikwa kama tunavyohubiriwa; bali walijaribu kulizika likiwa bado lina pumzi; na sasa limeamua kuamka. Baadhi yetu, tumejitolea kuwa watetezi wake wa mwisho!
Credit to: Mwanahalisi: http://www.mwanahalisi.co.tz/azimio_la_arusha_ccm_ondoeni_matanga
No comments:
Post a Comment