Na. LUANDA K.S.
KATIKA moja ya ahadi kumi za mwana-TANU; kila mwana-TANU alilazimika kuapa kuwa atakuwa tayari kwa namna yoyote ile kupambana na hatimae kuwashinda adui umasikini, maradhi na ujinga. Mwalimu Nyerere akiwa kama kiongozi mkuu wa TANU aliingia uwanjani kwa nguvu zake zote kuandaa mikakati na kusimamia utekelezaji wa kupambana na maadui hao, hadi kutufikisha pale alipotuachia alipong'atuka uongozi wa nchi yetu.
Ili kupambana na maadui hawa Mwalimu aliweza kupitisha maazimio tofauti kama vile lile la Azimio la Musoma la mwaka 1974 "Elimu kwa wote" ili kupambana na adui ujinga. Nyerere aligundua kuwa hata wazee ni wengi wasiojua kusoma na kuandika; akaanzisha "Elimu kwa watu wazima". Tulifikishwa mahali pazuri kitakwimu duniani kuhusu wasojua kusoma na kuandika. Makala hii itajitahidi kuungana na hayati Mwalimu Nyerere katika juhudi zake za kupambana na adui ujinga.
Elimu ni ufunguo wa maisha, ni nembo na msemo ambao hautapingwa na yeyote yule anayejua umuhimu wa elimu. Kwa bahati Nyerere alikuwa ni Mwalimu na alilijua hili. Elimu kuwa ni ufunguo pekee wa maisha ni dawa tosha kwa maadui wote wa taifa letu. Ni hivi, tukisoma, tutaelevuka, tutaepukana na maradhi na tutatumia elimu yetu kuutokomeza umaskini na vile vile tutazijua haki zetu hivyo hatutakubali kudhulumiwa. Hii ndio sababu inayonifanya nimuenzi hayati Mwalimu Nyerere kwa azimio la Musoma.
Ni wazi kuwa Mwalimu Nyerere aliienzi elimu, hakuishia kusisitiza elimu ya msingi tu, bali sekondari na hata vyuo vikuu na ili kutufagilia njia tufike huko, akaondoa kero katika elimu. Ni wazi kuwa tangu tupate uhuru miaka 39 iliyopita tunao madaktari bingwa wazalendo ambao ni matunda ya juhudi za Mwalimu. Cha kusikitisha ni pale shujaa huyu alipokosa kuyavuna matunda ya jasho lake pale alipougua na kupelekwa London ambako tunaamini hakuna yeyote yule aliyemuhudumia Mwalimu ambaye alisoma katika joto la wana-TANU huko London.
Mzalendo Mwalimu aliipenda sana nchi yake na kwa kujua (kutokana na elimu aliyokuwa nayo) umasikini wa Watanzania alijitahidi kuhakikisha kuwa kila shilingi itakayotumika ni kwa faida yetu Watanzania, alikemea na kuchukizwa mno na matumizi mabaya ya fedha za raia masikini wa Kitanzania. Sijasema kuwa kumpeleka London ni matumizi mabaya, bali tumuangalie Mwalimu msimamo wake tangu wakati huo na nini kilitumika katika hiki kipindi kigumu cha Septemba na Oktoba kwa Watanzania.
Nahisi kuwa matumizi yaliyofanywa kwa kipindi hiki kigumu yameshindwa kuyaenzi manukato mazuri ya jasho la Mwalimu pale alipotembea kutoka Musoma hadi Mwanza kuunga Azimio la Arusha.
Nasema hayo kwa sababu ni mamilioni mengi ya fedha za walalahoi ambayo yametumika tangu matibabu hadi tulowalipia wahudumu na waangalizi wa kifamilia na kiserikali katika kujikimu kuishi London kwa kipindi chote walichobahatika kuishi huko. Kama Mwalimu angetibiwa Muhimbili kama wazalendo wengine, pesa zilizotumika huko zingeweza kukarabati Muhimbili kwa asilimia kubwa zaidi. Kwa kufanya hivyo, tungemuenzi Mwalimu kwani aliuthamini msemo usemao "mtu kwao".
Tungekarabati kwetu na vile vile tungeweza kuwathamini wataalamu wetu. Lakini ni kiasi gani cha fedha ambacho kimeachwa London na ni Mtanzania gani atafaidika na pesa hizo? Mwalimu alisisitiza kufaidi kilicho chetu!
Kama kile kijumba tu ulipohifadhiwa mwili wa Hayati Mwalimu Nyerere uwanja wa Taifa kiligharimu shilingi milioni 32 pesa za Kitanzania, ni mamilioni mangapi yaliyotumika katika shughuli yote? Hii inaonesha sura gani kwa wananchi wa Ubungo wanaokosa maji kwa kukosekana milioni kidogo za kubadilisha mfumo chakavu wa maji ulowekwa toka enzi ya mkoloni?
Milioni thelathini na mbili zingeweza kuwaondolea adha ya kukosa dawa wananchi wa vijiji vya Ujamaa kama sita hivi kwa karibu mwezi na nusu. Labda zingeweza kujenga mitaro ya maji machafu maeneo ya Manzese na Tandale Uzuri ili kuondoa hali ya uchafu uliokuwepo maeneo hayo au labda hata zingeweja kutumika kuunda Tume kuchunguza mauaji ya Mwembechai.
Kwa kifupi ni kwamba, tunayo matatizo mengi yanayowagusa Watanzania ambayo utekelezaji wake ni mgumu au umekwama kwa ngonjera ya serikali haina pesa. Inapotokea kuwa raia wanapoteza maisha kwa kukosa dawa, wanafunzi hawana mahali pa kusomea, raia hufa kwa kukosa chakula, na asilimia kubwa ya Watanzania wanakosa maji safi, achilia mbali nishati kama vile umeme na barabara nzuri, lakini mamilioni mengi huenda hivi hivi kwa vitu ambavyo tungweza kuviepuka, tunajenga picha kuwa serikali haitaki.
Kwa mfano, iweje rahisi kujenga kibanda cha muda kwa shilingi milioni zaidi ya thelathini kwa siku tatu tu; serikali hiyo hiyo ikashindwa kuwalipa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Africa Mashariki? Au kuliondoa tatizo sugu la maji maji safi Ubungo na Mbagala ambako ni siku nyingi sasa na huenda kisigharimu kiasi hicho cha mamilioni?
Kasoro nyingi zimejitokeza katika ugonjwa, kifo na hatimae mazishi ya marehemu Mwalimu Nyerere. Naweza kusema kuwa ili kuzificha kasoro hizo likatafutwa neno takatifu ili kuziba nyufa zote zilizojitokeza. Neno hilo ni "kumuenzi Mwalimu". Mfano utakapohoji umuhimu wa kupoteza mamilioni ya shilingi kujenga kibanda ambacho baadae kimebomolewa utaonekana humuenzi Mwalimu.
Kwa vile tumesikia kuwa kuna mamilioni mengi ya shilingi ambayo hutolewa kama rambirambi kutokana na msiba huu, nashauri kuwa hizo rambirambi zingetumika katika kuboresha huduma za jamii. Nasema hivyo kwa sababu zifuatazo:
Ilikuwa ni rahisi kwa Mwalimu kuacha kazi (yaani kuacha mshahara kama alivyosema Bwana Keenja) mwaka 1954 kwa ajili ya kutumikia Watanganyika. Vile vile tutautumia moyo huo wa Mwalimu wa kutoa kilicho chake kwa ajili ya manufaa ya taifa hili.
Mwalimu alikuwa ni baba wa taifa zima, hivyo rambirambi hizo ni kwa taifa zima. Zitumike kuhudumia wafiwa ambao ni Watanzania. Pamoja na kuwa wafiwa wamechangishwa, hii ni mila yetu kuchangia mazishi, na haituzuilii kufanyika kwa rambirambi kutoka kwa majamaa, rafiki na majrani zetu na baba yetu.
Katika hali ya kawaida, madeni yaliyoachwa na hayati hulipwa kutoka mfuko wa rambirambi, iwapo mfuko huo haukutosheleza ndipo wana ndugu huchangia. Mwalimu ameacha deni kubwa nalo ni kiu yake ya kuona kuwa hali ya maisha ya Mtanzania inakuwa hatua mbali na maadui kama vile ujinga, maradhi na umasikini. Naomba ichukuliwe sehemu za mfuko huo ikatatue tatizo la maji Pugu shuleni ambako hakuna maji safi kwa jamii ile, au hata sehemu yoyote ile, kama ni sehemu ya kulikabili deni la hayati.
Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeziona pole tulizotumiwa Watanzania ambazo zimepokelewa kwa niaba yetu na Mheshimiwa Rais Mkapa kutoka sehemu mbalimbali duniani zimetufikia. Kinyume chake tutakuwa tumekosa baba; hekima zake na kupuuza aliyotufundisha. Tusimuenzi mwalimu kwa kuimba tu, tukaishia kunesanesa kwa utamu wa vinanda badala ya kunesanesa kwa mvuto wa utamu wa kisima na lulu ya upendo iliopotea!
No comments:
Post a Comment