Na Fredy Azzah, Mwananchi.
Watu waliopata fursa ya elimu wakati wa Mwalimu Julius Nyerere , mpaka leo wanajivunia elimu hiyo, hali ambayo ni tofauti kabisa na ile wanayopata watoto wetu wa leo.
Ni vigumu kumzungumzia Mwalimu Julius Nyerere leo bila kutaja mchango wake kwenye sekta ya elimu nchini.
Inawezekana kuwa, taaluma yake ya ualimu ndiyo iliyomfanya awe na hamu ya kuhakikisha anaisaidia sekta ya elimu wakati wote wa uhai wake.
Juhudi zake za kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata elimu zilianza hata kabla ya uhuru wa Tanganyika. Kwa mfano, Desemba 20 mwaka 1956 alipopata fursa ya kuzungumza mbele ya Umoja wa Mataifa (UN), kati ya mambo aliyoyazungumzia ilikuwa ni suala la ubaguzi kwenye kupata fursa ya elimu kati ya watoto wa Kitanzania na wale wa Wakoloni.
“Nchini Tanganyika elimu inatolewa kibaguzi. Watoto wote wa Kizungu na wa Kiasia wanakwenda shule ambapo ni asilimia 40 tu ya watoto wa Kiafrika wanaokwenda shule.” Inaeleza sehemu ya hotuba.
Hotuba hii inaweza kutafsiriwa kuwa moja ya viashiria kuwa Mwalimu Nyerere alijali suala la elimu, kwani baadhi ya watu waliopata fursa za kuzungumza mbele ya baraza hilo kumbukumbu hazionyeshi kama walizungumzia suala la elimu.
Japhet Kirilo ndiye alimtangulia Mwalimu Nyerere kwenda kuzungumza UN, Julai 21 mwaka 1952.
Kirilo alitumwa na Chama cha Raia wa Meru (Meru Citizens Union) kwenda UN kudai ardhi ya Wameru iliyokuwa imeporwa na wakoloni, Waingereza.
Maombi ya Kirilo hayakufanikiwa na mpaka leo, eneo kubwa la Meru bado lina mgogoro mkubwa wa ardhi na kubwa zaidi ikiwa imeshikiliwa na watu waliopewa tangu nyakati hizo za wakoloni.
Vivyo hivyo, hata kwenye sekta ya elimu iliyoanza kupigiwa kelele kabla ya taifa hili kupata uhuru, mpaka leo inakabiliwa na changamoto lukuki.
Hata baada ya uhuru, Mwalimu Nyerere aliendelea kupigania elimu, kwenye hotuba zake mbalimbali alizozitoa hakuwa cha kuzungumzia bilasuala la elimu.
Akizungumza juu ya Elimu ya Kujitegemea mwaka 1967, Mwalimu Nyerere alisema: “Kwa kweli nchi huru ya Tanzania ilirithi mtindo wa elimu ambayo kwa njia nyingi ilikuwa haitoshi wala haifai kwa haja za nchi hii. Lakini kulikodhihirika mapema zaidi ni kutokuridhisha kwa elimu.
Elimu iliyotolewa ilikuwa finyu. Mwezi Desemba 1961, watu wenye elimu ya kutosha walikuwa wachache mno wala wasingetosha kuendesha Serikali ya siku zile, ukiachilia mbali kazi zingine kama za mipango ya maendeleo zilizokuwa muhimu zaidi.
Idadi ya watoto waliokuwa shule mwaka 1961 haikuwa kubwa ya kutoa matumaini kwamba hali hii ingeweza kurekebishwa haraka.
Zaidi ya hayo, elimu iligawiwa kwa mataifa, ambapo msingi wa madai yetu yote ya uhuru ulikuwa ni kulaani kabisa ubaguzi wa rangi.”
Hadi leo ukijaribu kusoma hotuba zake, utabaini kuwa falsafa yake kwenye suala la elimu, ilijikita zaidi kwenye elimu ya kujitegemea na ile ya watu wazima.
Ama kwa hakika kwa wakati ule, elimu ya kujitegemea iliwasaidia wengi kuwa na mawazo ya kujitegemea wao pamoja na kuliendeleza taifa huku ile ya watu wazima ikiwakomboa mamilioni waliokosa fursa ya elimu wakati wa utawala wa mkoloni.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, mawazo ya Mwalimu kuhusu msingi wa elimu kwa watu wazima, yaliendana sambamba na yale ya wataalamu kama kina Malcom Knowles na J Roby Kidd.
Katika kitabu cha Elimu ya Kujitegemea, Mwalimu Nyerere anasema kati ya makosa matatu yaliyokuwa kwenye elimu ya kikoloni ambayo tuliirithi ni ubaguzi wa rangi katika kutoa elimu.
“Mara tu baada ya uhuru ulianzishwa mpango wa kuunganisha kabisa shule za mataifa yote na ubaguzi kutokana na dini pia ukakomeshwa.
Sasa, mtoto wa Tanzania anaweza kusoma katika shule yoyote ya Serikali, au shule yoyote inayosaidiwa na Serikali katika nchi hii, bila ya kujali rangi au dini yake na bila hofu kwamba gharama ya elimu yake ni kufundishwa dini nyingine,” inaeleza sehemu ya kitabu hicho.
Hata hivyo, wadau wa elimu wanasema kuwa, kwa sasa sifa hii imefutika kutokana na shule za kata ambazo zinawalazimu watoto kusoma shule zilizo kwenye maeneo yao tofauti na zamani ambapo walikuwa wanapangiwa hata nje ya mikoa yao.
Mmoja wa watu waliofanya kazi kwenye sekta ya elimu chini ya Mwalimu Nyerere, Dk Maria Kamm, aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru iliyoko Moshi, Kilimanjaro kati ya mwaka 1970 mpaka 1992 anakiri hilo.
Anasema aliweza kuiongoza shule hiyo kwa mafanikio kutokana na sera ya kujitegemea ambayo ilikuwa ikitekelezwa kwa vitendo chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere. “Elimu ya kujitegemea ilijenga jeuri yangu, ilifanya nyote mpate elimu sawa, wote mlikuwa sawa, sote tulifanya kazi bila upendeleo,” anaeleza.
Anaongeza: “Kujitegemea siyo siasa ni kawaida ya Mwafrika, bila kuwa na sera na viongozi kufuatilia utekelezaji wake hatutafika mbali.”
Mwalimu Nyerere pia alichangia ukuaji wa elimu ya juu kwa misingi ya kuwa chachu ya maendeleo na fikra.
Wakati anakifungua Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam mwaka 1970 alisema, “Chuo kikuu ni taasisi ya elimu ya juu ambayo kwayo watu wanapata mafunzo ya kupanua wigo wa uelewa wao, fikra huru na sahihi, uchambuzi wa matatizo na kuyatatua kwa kiwango cha juu.”
Katika moja ya hotuba alizotoa mwaka 1981, Mwalimu Nyerere alisema watu waliopata fursa ya elimu wana wajibu wa kurudi na kulipa fadhila kutokana na kile ambacho wengine wamewafanyia.
Alisema watu hao ni sawa na wale waliopewa akiba yote ya chakula ili wapate nguvu na kwenda kutafuta kingi zaidi wawaletee wanakijiji wenzao.
Mwalimu Nyerere alisema kuwa, watu hao wasipotimiza wajibu huo, watahesabika kama wasaliti.
Wakati tukifanya kumbukumbu ya miaka 14 tangu kufariki kwake, hatuna budi kukumbuka maneno yaliyomo kwenye hotuba yake ya mwaka 1967 alipokuwa akizungumzia elimu ya kujitegemea.
Alisema: “Elimu inayotolewa Tanzania, kwa watoto wa Tanzania, haina budi itosheleze haja za Tanzania. Haina budi ipande mawazo ya taifa la kijamaa tunalotaka kulijenga.
Haina budi ikazanie kufunzwa kwa wananchi wanaojivunia uhuru na kujitegemea kwa maendeleo yao wenyewe, na ambao wanafahamu faida na shida za kushirikiana.
Elimu haina budi ihakikishe kwamba wale waliosoma wanajitambua kwamba ni sehemu ya taifa na kwamba kwa kuwa wamepata nafasi zaidi, basi wajibu wao kwa taifa ni mkubwa zaidi.
Hili si jambo linalohusu masomo na utaratibu wa shule peke yake. Maadili hufunzwa nyumbani, shuleni na vijijini: Maadili hufunzwa na mazingira ya mtoto anamoishi.
Lakini haina maana shule zetu kukazania kufunza maadili na maarifa yaliyokuwa yanafaa zamani au yanayowafaa raia wa nchi zingine na kumbe elimu yenyewe inapendekeza kuendelezwa kwa hali tuliyoirithi ya kuwa na tofauti baina ya raia na raia wengine.
Yafaa watoto wetu waelimishwe kuwa raia wa kesho na watumishi wa wananchi walio sawa, katika taifa tunaloliunda.”
Credit to: http://www.mwananchi.co.tz/Makala/Maoni-ya-Nyerere-na-uhalisia-sekta-ya-elimu-leo/-/1597592/2033104/-/item/0/-/yldt65z/-/index.html
No comments:
Post a Comment